WAKATI Serikali ya Zanzibar ikiendelea kujenga viwanja vya michezo kisiwani hapa, wadau wa mpira wa kikapu wamelia na ukosefu wa viwanja.
Wadau hao wamesema viwanja vya mchezo huo vipo vichache na wakati mwingine havipatikani kabisa, hivyo huwalazimu kusitisha mazoezi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu ya Stone Town, Kamal Mohamed, amesema viwanja vya mchezo huo bado ni vichache kwa Zanzibar.
Akitolea mfano timu hiyo, amesema inatakiwa kushiriki mashindano ya JMK Park Open yanayofanyika Dar es Salaam mwezi Desemba, lakini hadi sasa timu hiyo ipo tu bila ya kufanya mazoezi.
“Tunatambua kwa sasa viwanja vyote vipo chini ya mwekezaji, hivyo tunaiomba Serikali kumsimamia kutoa utaratibu wa upatikanaji wa viwanja hivyo,” amesema.
Amesema, awali walikuwa wanatumia viwanja hivyo kufanyia mazoezi bila malipo yoyote huku akisisitiza mchezo huo hauwezi kukua endapo hawatopata sehemu ya kufanyia mazoezi.
Kamal alisisitiza timu hiyo inahitaji kujiandaa na mashindano hayo kwani wao ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo.
Amesema, Serikali kumpa viwanja mwekezaji kwa ajili ya usimamizi ni hatua kubwa kwa maendeleo ya taifa kwa maana hiyo ni wakati wa kutoa muongozo unaopaswa kufuata juu ya utumiaji wa viwanja.
Pia, Kamal ameiomba Serikali kuwa mwekezaji huyo atoe muongozo unaozingatia hali za timu na ajira kwa vijana wenye uwezo wa kusimamia michezo kulingana na kada yake.
Hivyo, wameiomba serikali kutoa muongozo maalumu unaopaswa kufuatwa na timu hizo kupata viwanja hivyo kuvitumia ili watoto wasikae bure mitaani.
Serikali ya Mapinduzi kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, imeingia mkataba wa miaka 15 na kampuni ya Bahari Leisure kuendesha viwanja vya michezo Unguja na Pemba.
