Mbeya. Kazi imeanza, lazima kieleweke. Ni kauli ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa ikielezea kurejea kwa shughuli zake za kisiasa, huku kikiomba wananchi na wafuasi wake kukisapoti.
Chadema haijafanya shughuli zozote za kisiasa kwa takribani mwaka mmoja tangu ilipofungiwa na Mahakama Kuu, kufuatia kuwapo kwa kesi ya mgawanyo wa mali na juzi Aprili 15 kilifunguliwa kuendelea na majukumu yake.
Akizungumza jana Aprili 18, 2026 wakati wa usafi na ufunguzi wa ofisi ya Kanda iliyoambatana na kupandisha bendera ya chama hicho, Katibu wa Chadema Kanda hiyo, Grace Shio alisema kwa sasa chama hicho kipo mikononi mwa wananchi, akiomba sapoti yao katika mwendelezo wa kupigania haki.
Alisema kwa muda ambao hawakufanya shughuli, wananchi walikosa haki zao na chama kwa ujumla katika kutetea na kudai maslahi ya wananchi akieleza kuwa kufunguliwa kunarejesha upya.
Alisema Chadema imepitia kipindi kigumu ambapo hawawezi kumsahau Mwenyekiti wao Taifa, Tundu Lissu anayeendelea kusota rumande.
“Wote tufahamu haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, hatuwezi kukubali hali hii iendelee, lazima tulinde misingi ya haki na demokrasia kwa kila mmoja.
“Leo tunaporejea kuendelea na shughuli za chama, hatuji kwa kuvunjika moyo bali tunakuja tuliothibitishwa na mapambano, ushindi wa Aprili 15 si wa chama pekee bali hata demokrasia na wananchi wanaoamini katika haki,” alisema Grace.
Aliwaomba viongozi kuanzia ngazi za msingi hadi Taifa kuendelea kuungana bila kugawanyika bali kushikamana na kuwaelekeza viongozi kanda hiyo kufungua ofisi zote kwenye maeneo yao, ili kuendelea na shughuli za chama na kuandaa ratiba za mikutano ya hadhara, usajili wa wanachama kupitia mfumo wa kidijitali.
Alisema Chadema itaendelea kupigania haki za Watanzania wote bila woga, akieleza kuwa wanaodhani wanaweza kuwanyamazisha milele, sauti ya haki haiwezi kufutika na wako tayari kutetea Tanzania kwa haki na usawa na kuwashukuru wadau ambao wamekuwa pamoja na chama hicho.
Wanachama na wafuasi wa Chama mcha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa wakiwa katika ofisi za Kanda hiyo zilizopo Mtaa wa Kdege jijini Mbeya baada ya kufungua ofisi hiyo kuendelea na majukumu kufuatia kufunguliwa kwa chama hicho Aprili 15.
“Tunaomba Mwenyekiti wetu Lissu aachiwe huru bila masharti, tunaomba viongozi wote akiwamo Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Iringa, Ibrahim Nyovela na wanaharakati wengine kama Mdude Nyagali warejeshwe wakiwa salama,” alidai.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Chonya Elisha alisema kwa sasa kazi inaanza upya.
Alisema uongozi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya umejipanga vyema kuendeleza walipoishia kwa nguvu mpya akiwaomba wafuasi kujiandaa kwa shughuli kubwa za kukipambania chama hicho na Tanzania kwa ujumla kwenye misingi ya haki.
“Watu wameonewa, wamedhulumiwa, tulizuiwa kukutana, kutoonana, kutoa maoni kutokana na kukosa utawala bora katika nchi na sasa furaha imerudi upya lazima turudi kwa nguvu.”
“Tunaanza kuidai katiba mpya kwa moto mkubwa, sisi Baraza la Vijana (Bavicha) tutakuwa msitari wa mbele kuanzia mkoa hadi Taifa na Mbeya ndio tutaongoza kampeni hii ili watu watendewe haki na kupata utawala wa kisheria, mwaka huu lazima kieleweke,” alidai Elisha.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama hicho Taifa (Bawacha), Elizabeth Mwakimomo alisema walikuwa na haki zote kama wanawake wengine lakini walinyimwa haki yao ya msingi katika kujijengea uwezo na kukutana kundi hilo.
“Niwaombe sana tuungane kwa nguvu kilindi hiki kuhakikisha Mwenyekiti wetu Lissu anatoka gerezani na tunaomba mamlaka zimuachie huru aweze kuungana na wanachama wake katika majukumu ya chama, Bawacha tutapambana kudai haki hii ya kiongozi wetu,” alisema Elizabeth.
