Tanzania yang’ara Tanfoam Marathon Arusha

Wanariadha wa Tanzania wamefanikiwa kupeta katika mashindano ya Tanfoam Marathon, baada ya kukata utepe kwa upande wa kilomita 42 na 21 mbele ya wanariadha kutoka Kenya na Uganda.

Mbio hizo msimu wa pili zilizokimbiwa katika Barabara ya Njiro na kuishia viwanja vya General Tyre jijini Arusha, zilishirikisha zaidi ya wakimbiaji 1200.

Katika mbio za kilomita 21 wanaume, wanariadha wa Tanzania walionesha ubabe mapema, ambapo Boay Maganga wa klabu ya Talenti aliibuka mshindi akimaliza kwa muda wa 1:04:50, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Protas Gabriel kutoka Singida aliyetumia muda wa 1:05:04, wakati Daniell Sinda wa JKT akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 1:05:21.

Kwa upande wa wanawake katika mbio za kilomita 21, Magdalena Shauri wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliongoza tangu mwanzo hadi mwisho na kuibuka mshindi akitumia muda wa 1:11:36, nafasi ya pili ilikwenda kwa Failuna Matanga wa Talenti (1:14:23), huku Tunu Andrea wa JAKMA akimaliza wa tatu kwa muda wa 1:15:01.

Washindi wa kwanza katika mbio za nusu marathon kwa wanaume na wanawake walizawadiwa Sh5 milioni kila mmoja, huku washindi wa pili na wa tatu wakijinyakulia Sh2 milioni 2 na Sh1 milioni.

Mbio za kilomita 42 kwa wanaume, Modest Peter Kalist wa Ambassador Club aliibuka mshindi kwa muda wa 2:15:58, akifuatiwa na Mosses Mengichi kutoka Kenya aliyetumia muda wa 2:20:02, nafasi ya tatu ilichukuliwa na Jonathan Akankwasa kutoka Uganda kwa muda wa 2:20:23.

ARU 02

Kwa upande wa wanawake katika mbio za kilomita 42, Tanzania iliendelea kung’ara kupitia Vaileth Kigasi wa Talenti Club aliyeshinda kwa muda wa 2:42:10, nafasi ya pili ilichukuliwa na Mkenya Maureen Jepkoech (2:43:19), huku Edinah Too akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 2:44:16.

Washindi wa mbio kamili za marathon walipokea Sh6 milioni kila mmoja, huku washindi wa pili na wa tatu wakijipatia Sh2.4 milioni na Sh1.2 milioni.

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Mwenyekiti wa mbio hizo, Glorious Temu, alisema lengo la marathon hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha afya ya jamii kupitia mazoezi ya viungo, sambamba na kuendeleza mchezo wa riadha nchini.

Ameongeza kuwa, ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza linafanya jitihada kama hizo kuwa muhimu zaidi kwa sasa.

“Mbio hizi zinatoa jukwaa muhimu si tu kwa ajili ya afya, bali pia kwa wanariadha kujipima dhidi ya washindani kutoka nchi jirani,” amesema.

ARU 01

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Rogath Steven, aliipongeza Tanfoam Marathon kwa kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji na kuwaandaa wanariadha kwa mashindano ya kimataifa.

Pia amewataka waandaaji wa mbio nchini kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa za uandaaji wa mbio kuepuka rungu kutoka RT.

“Tanfoam Marathon imeweka mfano mzuri kwa kufikia viwango vya kimataifa. Waandaaji wanapaswa kufuata taratibu, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa,” amesema.

Mgeni rasmi na mwakilishi wa mdhamini mkuu, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya CRDB, Cosmas Sadat, amesisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kukuza riadha na kuitangaza Tanzania kimataifa.

“Kama CRDB, tunaendelea kujitolea kusaidia michezo kwa kudhamini matukio yanayowapa wanariadha fursa ya kushindana, kujipatia kipato na kukuza vipaji vyao,” amesema.