Chomelo azidi kutesa Ligi ya Uturuki

KIUNGO mshambuliaji Mtanzania, Ramadhan Chomelo ameendelea kuonyesha ubora wake katika kikosi cha Despas Enerji inayoshiriki Ligi Kuu ya Walemavu licha ya kujiunga na timu hiyo dirisha dogo.

Chomelo alijiunga na chama hilo katikati ya msimu akitokea Konya Amputee ya ligi hiyo alipohudumu kwa misimu mitatu mfululizo.

Tangu ajiunge kikosini hapo, amecheza jumla ya mechi nne akihusika moja kwa moja katika mabao matano, akifunga bao moja na kutoa asisti nne.

Takwimu hizo zinamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa ndani ya muda mfupi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo amesema alitamani kufanya zaidi ya alichoonyesha akiwa na kikosi cha Despas lakini changamoto za nje ya uwanja zilimwangusha.

“Kama isingekuwa changamoto za nje ya uwanja, naamini ningekuwa nimefunga mabao mengi hivyo msimu umeisha kwangu haujawa mzuri sana wala mbaya sana,” amesema Chomelo na kuongeza;

“Imebaki mechi moja ya kumaliza msimu na naamini kama nitakuwa sawa basi msimu ujao unaweza kuwa bora kwangu.”

Rekodi za Chomelo katika misimu mitatu, wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 20 akifunga mabao saba na asisti 16, msimu 2023/24 alicheza mechi 21 akifunga mabao manne na asisti tisa na msimu jana aliweka kambani mabao matano na asisti 11.