Sinza kujengwa upya, wamiliki waibua maswali

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikibainisha mpango mpya wa 2026/2046 wa kuliendeleza eneo lote la Sinza jijini Dar es Salaam, wamiliki wa nyumba katika eneo hilo wamehoji ni wapi watakwenda kuishi mpango huo ukianza.

Pia, wamehoji ni namna gani wamiliki wanane wataunganisha viwanja vinane ili kupata ukubwa wa kiwanja kimoja na katika eneo litakalounganishwa ni nani atakuwa mmiliki?

Baadhi yao wametaka wapewe Sh1 bilioni ili kuyaachia maeneo yao kwa mwekezaji, wengine wakitaka Sh3 bilioni.

Mpango huo wa kuiendeleza Sinza mpya ni wa miaka 20 utaanza 2026, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa ndiye msimamizi, ikilenga kuwa na eneo jumuishi Sinza.

Mpango huo utahusu kujenga maghorofa ya makazi na biashara  huku maeneo ya huduma za jamii kama shule na hospitalini yatabaki palepale lakini yataboreshwa kuwa ya ghorofa.

Hayo yameelezwa leo Jumapili, Aprili 19, 2026 na Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Emily Mwasogye katika kikao na wamiliki wa maeneo hayo.

Afisa ardhi wa wizara, Emily Mwasogye akifafanua mpango wa kuendeleza Sinza mpya

Mwasogye amesema ardhi ya Sinza imejaa, hivyo Serikali inakwenda kulipanga eneo hilo kwa kwenda juu kujengwa maghorofa.

“Tunataka kuwa na mji jumuishi ambao utapunguza watu kwenda kupata huduma katika maeneo mengine.

Akifafanua namna mpango huo utakavyokuwa, Mwasogye amesema wenye maeneo ya Sinza A-C, wamiliki wanane wataunganisha viwanja kutokana na udogo wa maeneo hayo na kufafanua watakubaliana kuingia mkataba na mwekezaji wa kugawana asilimia 50 kwa 50.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, wamiliki wanane wataunganisha eneo lao na kuwa kiwanja kimoja, akifafanua viwanja vya Sinza ni vidogo na kwa mpangilio wa majengo itabidi viwanja vinane kuunganishwa ili kiwe kimoja hasa katika kitalu A hadi C.

Wale wa kitalu D na E mpango wa kuunganisha viwanja hautawagusa kutokana na aina ya udongo wao kutokidhi kujenga ghorofa refu zaidi.

Amesema katika kitalu A hadi C kuna maeneo yatajengwa ghorofa 20 hadi nane wakati yale ya kitalu D na E yatajengwa ghorofa nne hadi mbili kulingana na udongo.

Amesema kuna njia tatu kwa wamiliki kuzifanya katika mradi huo, kwanza ni kugawana asilimia 50 kwa 50 kati ya mmiliki na mwekezaji, au kuuza eneo hilo kwa mwekezaji na njia nyingine ni kulipangisha eneo lake katika mradi huo.

Wamiliki Sinza wakishiriki katika kikao cha kuboresha makazi yao

Zuwena Athuman ambaye ni mmiliki wa kiwanja 748A amehoji watakapokwenda kuishi katika kipindi chote cha mradi.

Akijibu hilo, Mwasogye amesema kama ujenzi utachukua miaka mitatu au miwili, basi mmiliki katika eneo husika atapangishiwa nyumba na mwekezaji katika kipindi chote cha mradi.

“Kama alikuwa na biashara, pia atasema kwa mwaka iliingiza kiasi gani,” amesema.

Mmiliki mwingine alihoji endapo kwa wale wamiliki ambao watatakiwa kuunganisha viwanja ili vifike vinane, ikitokea watatu wakagoma kuunganisha nini kitafuata.

Akijibu hilo, amesema katika hatua ya kwanza ya miaka mitano kutakuwa na majadiliano.

Hata hivyo, mpango wa kuunganisha viwanja ulionekana kutoeleweka kwa wamiliki, wakihoji ni vipi watu wanane wawe wamiliki katika eneo moja lililoendelezwa.

Salama Ismail wa Sinza B amehoji endapo wamiliki watano watakubali kuunganisha na watatu kugoma, nini kitafanyika.

Akijibu hilo, Emily amesema kutakuwa na kipindi cha majadiliano na makubaliano ya kisheria katika hilo.

Hata hivyo, wizara imetoa nafasi kwa wamiliki wenye uwezo wa kuendeleza maeneo yao bila kuhitaji mwekezaji katika mkakati huo, kushirikiana kuyaendeleza katika mpango huo kipindi cha mradi.