Arusha. Kikundi cha Kuendeleza Vipaji na Ubunifu wa Viziwi nchini (Kikuvuvita) kimeanzisha mpango wa kuchapisha jarida la lugha ya alama za magonjwa, litakalosaidia kuboresha mawasiliano kati ya watu wenye uziwi na wahudumu wa afya.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Aprili 19, 2026 Mwenyekiti wa Kikuvuvita mkoani Arusha, Agrey Lyimo amesema kikundi hicho kinahitaji Sh100 milioni kufanikisha uchapishaji wa jarida hilo, linalolenga kuondoa changamoto ya mawasiliano inayowakabili wanachama wao wanapohitaji huduma za afya.
Lyimo amesema ubunifu huo umetokana na malalamiko ya watu wenye uziwi kushindwa kupata huduma stahiki kutokana na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vya afya.
“Jarida hili litasaidia madaktari na wauguzi kuelewa dalili na mahitaji ya wagonjwa wenye uziwi bila kutegemea mkalimani, hivyo kulinda pia usiri wa mgonjwa kama maadili ya taaluma ya tiba yanavyoelekeza,” amesema.
Ameongeza kuwa utegemezi wa wakalimani mara nyingi huathiri faragha ya mgonjwa mwenye uziwi na unaweza kudhalilisha utu wake, hali inayoweza kuepukwa kwa matumizi ya nyenzo hiyo mpya ya mawasiliano.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 14 ya Watanzania wenye umri wa miaka mitano na zaidi wanaishi na ulemavu. Kati yao, asilimia 10.2 wana ulemavu wa kusikia huku asilimia 5.7 wakiwa na ulemavu wa kuzungumza.
Lyimo amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuwekeza katika suluhisho bunifu zitakazowezesha makundi hayo kupata huduma muhimu kwa usawa, ikiwa ni pamoja na huduma za afya.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida, Dk Emmanuel Malange, amepongeza ubunifu huo akisema utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watu wenye uziwi.
Amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wahudumu wa afya kwa kuwapatia mafunzo ya lugha ya alama ili waweze kuwahudumia wagonjwa wote kwa usawa na kuzingatia misingi ya usiri wa taarifa za mgonjwa.
