Meli iliyobeba saruji yazama Zanzibar, wanne wapotea

Dar es Salaam. Watu wanne kati ya 14 wanatafutwa baada ya meli ya MV Jozani II kuzama maji katika maeneo ya Pwani ya Tanga usiku wa kuamkia Aprili 17, 2026.

Taarifa kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), katika ajali hiyo, watu 10 wameokolewa na wanne wanaendelea kutafutwa.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, jumla ya mabaharia 14 walikuwa ndani ya meli wakati wa tukio hilo ambapo kati yao, mabaharia 10 waliokolewa salama na kufikishwa katika Bandari ya Tanga.

“Mabaharia wanne wameripotiwa kupotea wakiwemo nahodha wa meli, Mhandisi Mkuu wa Meli pamoja na wafanyakazi wengine wawili,” imeeleza taarifa hiyo ya Tasac. 

Meli hiyo iliyosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), inamilikiwa na Kampuni ya Al Ghubra Marine Services, iliondoka Bandari ya Tanga Aprili 16, 2026 saa 1:40 usiku ikiwa imebeba mzigo wa saruji takribani tani 800 kuelekea Zanzibar.

“Katika hatua za haraka za uokoaji, meli iliyokuwa karibu eneo la tukio, MT Tom Emma, ilifanikiwa kuokoa manusura.

 
“Aidha, Tasac imepeleka boti ya utafutaji na uokoaji (SAR) kushirikiana na vyombo vingine katika operesheni inayoendelea ya kuwatafuta waliopotea,” imeeleza taarifa hiyo. 

Hata hivyo, Tasac kwa kushirikiana na ZMA na mamlaka nyingine zinaendelea na uchunguzi wa tukio hili. 

Ingawa, uchunguzi wa awali unaonesha kuna mambo kadhaa yanayohitaji kuchunguzwa kwa kina, ikiwemo hali ya uthabiti wa meli, upangaji wa mzigo, hali ya hewa wakati wa tukio, pamoja na uwezekano wa hitilafu za kiufundi.

Aidha, Shirika linaendelea kutoa wito kwa wadau wote wa sekta ya usafiri wa majini kuzingatia kikamilifu taratibu na kanuni za usalama ili kuzuia ajali kama hiyo.