Wananchi wafugaji kunufaika na mashine ya kusaga

Simanjiro. Wananchi wa jamii ya wafugaji katika kitongoji cha Noomunyi, kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameondokana na adha ya kutembea umbali wa hadi kilomita 15 kufuata huduma ya kusaga na kukoboa nafaka, baada ya kupatiwa mashine ya kisasa.

Mashine hiyo imetolewa na mdau wa maendeleo wa wilaya hiyo, Taiko Ole Kulunju, ikiwa ni jitihada za kuboresha maisha ya wanawake na kuongeza muda wa kushiriki shughuli za kiuchumi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Aprili 19, 2026, Taiko amesema uamuzi wa kutoa msaada huo umetokana na ombi la muda mrefu kutoka kwa wanawake hao waliokuwa wakipata changamoto ya kusafiri umbali mrefu kusaga mahindi.

“Wanawake katika jamii ya wafugaji wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa familia. Haikuwa sahihi waendelee kuteseka kwa kutembea umbali mrefu kwa huduma hii muhimu,” amesema.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Kaleya Mollel (wanne kulia) na mdau wa maendeleo Taiko Ole Kulunju (katikati) baada ya uzinduzi wa mradi wa mashine ya kusaga na kukoboa nafaka kwenye kitongoji cha Noomunyi, kata ya Loiborsiret. Picha na Joseph Lyimo

Amesema mahitaji hayo yaliwasilishwa tangu mwaka jana, na baada ya kulichambua, waliamua kutekeleza mradi huo ili kupunguza mzigo kwa wanawake hao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleya Mollel, amepongeza hatua hiyo akisema imeondoa kero ya muda mrefu kwa wakazi wa eneo hilo.

“Kwa niaba ya halmashauri, tunamshukuru mdau huyu kwa kuisaidia jamii yetu, hususan wanawake waliokuwa wakipoteza muda mwingi kufuata huduma ya kusaga,” amesema.

Mmoja wa wanufaika, Magdalena Leskary, amesema mashine hiyo imekuwa msaada mkubwa kwao kwani imewaondolea mzigo wa safari ndefu na hatarishi.

“Hapo awali tulikuwa tunatembea umbali mrefu kwenda kusaga unga na kurejea nyumbani, hali iliyotuchosha na kupoteza muda mwingi. Sasa tuna huduma karibu,” amesema.

Ameahidi kuwa watautunza mradi huo ili uwe endelevu na kuendelea kuwahudumia kwa muda mrefu.

Naye Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga, amesema upatikanaji wa mashine hiyo utawawezesha wanawake kutumia muda wao kufanya shughuli nyingine za uzalishaji na malezi ya familia badala ya kuupoteza wakiwa njiani kwenda kusaga nafaka.