Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza viongozi wa Serikali kuacha utaratibu wa kusimamia miradi wakiwa ofisini badala yake, waende moja kwa moja kwenye maeneo ya utekelezaji ili kujionea hali halisi ya miradi.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili, Aprili 19, 2026, wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa maji Chamwino, akisisitiza kuwa usimamizi wa karibu ni muhimu ili kudhibiti ubadhirifu na kuongeza uwajibikaji.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mkandarasi Megha Engineering kutoka India, kwa gharama ya Sh17.2 bilioni, ukilenga kuhudumia zaidi ya wakazi 60,000 wa kata za Msanga, Chamwino, Buigiri na Mtumba.
Dk Mwigulu amesema tabia ya viongozi kupokea taarifa za maendeleo ya miradi wakiwa ofisini imekuwa ikichangia kuwepo kwa miradi hewa na vitendo vya udanganyifu.
“Utaratibu huu wa kupokea taarifa ofisini wakati mwingine unasababisha kuwa na miradi mingi hewa na udanganyifu uliokithiri. Ni muhimu viongozi mfike maeneo ya miradi mjionee hali halisi,” amesema.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28, Chamwino Dodoma, Aprili 19, 2026. Kushoto ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Akimpongeza Waziri wa Maji (Juma Aweso) kwa kufuatilia miradi kwa kutembelea maeneo husika, Waziri Mkuu amesema hatua hiyo ni ya kuigwa na viongozi wengine.
“Nakupongeza Waziri wa Maji kwa mtindo wa kwenda ‘site’ moja kwa moja. Kumbuka kuna wakati kwenye mradi mmoja uliambiwa kisima kimepotea. Mambo kama hayo hayakubaliki,” amesema.
Aidha, ametoa onyo kwa makandarasi wanaotekeleza miradi ya Serikali, akisisitiza kuwa ni lazima walipe stahiki za wafanyakazi na wadai wengine kwa wakati.
Amesema mkandarasi yeyote atakayepokea fedha za mradi na kushindwa kulipa madeni, atachukuliwa hatua kali, ikiwamo kufungiwa kushiriki zabuni za Serikali.
Mkurugenzi wa Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji, Charles Mafie amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 28 awamu ya nne, inayotekelezwa katika maeneo ya Chamwino, Kiomboi, Singida, Manyoni, Chemba na Mvumi.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akifiurahia ngoma ya kikundi cha Makunga alipowasili Chamwino Dodoma kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28, Aprili 19, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Amesema mradi ulianza Aprili 2023 na hadi sasa umefikia utekelezaji wa asilimia 70.2, ukitarajiwa kukamilika Agosti 2026.
Mafie amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 7.7 za maji kwa siku, wakati mahitaji ya sasa ya maeneo hayo ni lita milioni 7.5, hali itakayowezesha kuwepo kwa ziada ya maji.
Amesema hadi sasa visima vinane vimechimbwa, hatua inayochangia kufanikisha upatikanaji wa maji kwa uhakika katika maeneo husika.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa mradi huo, ikiwamo kuchelewa kulipwa fidia.
Mkazi wa Chamwino, Mariam Nyembela amesema pamoja na matarajio ya kunufaika na huduma ya maji, bado hawajalipwa fidia ya maeneo yao yaliyotumika kupisha ujenzi na upanuzi wa mradi.
Amesema awali walipewa ahadi ya kulipwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, lakini hadi sasa hawajapata malipo yao, jambo linalowatia wasiwasi.
Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28, Chamwino Dodoma, Aprili 19, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
“Tuliahidiwa kulipwa kabla ya ujenzi kuanza, lakini hadi sasa hatujalipwa. Tuna hofu mradi utakamilika kabla hatujapata haki zetu,” amesema Mariam.
Akijibu hoja hiyo, Msimamizi msaidizi wa mradi huo, Titho Alex amesema uthamini wa mali za wananchi umeshakamilika na malipo ya fidia yatafanyika kabla ya kukamilika kwa mradi.
