Baba aua watoto wake saba kwa risasi, naye auawa

Marekani. Mwanaume aliyetambulika kwa jina la Shamar Elkins ameua watoto wake saba pamoja na mwingine asiye wa familia hiyo, katika tukio la kuwafyatulia risasi mjini Shreveport, jimbo la Louisiana, Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na kituo cha habari cha CBS, watoto hao walikuwa na umri wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka 14.

Polisi wa Shreveport wamesema tukio hilo lilitokea jana asubuhi, Aprili 19, 2026, na mshukiwa alifyatua risasi na kuwajeruhi watu 10 kabla ya kukimbia kwa kutumia gari lililoibiwa.

Msemaji wa Polisi wa Shreveport, Chris Bordelon, amesema baada ya msako mkali, askari walimfuatilia mshukiwa huyo na hatimaye kumpiga risasi na kumuua.

Wanawake wawili, akiwemo mama wa watoto waliouawa, wamelazwa hospitalini wakiwa mahututi kutokana na majeraha ya risasi.

Taarifa ya polisi imeeleza kuwa mshukiwa huyo alianza kwa kumpiga risasi mwanamke mmoja barabarani kabla ya kuelekea nyumbani, ambako aliwaua watoto wanane kwa risasi.

Katika tukio hilo, mtoto mmoja alinusurika baada ya kukimbilia nyumba ya jirani na kupiga simu polisi, huku mtoto mwingine akiruka kutoka juu ya paa kujiokoa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Akizungumzia tukio hilo, Meya wa Shreveport, Tom Arceneaux, amesema ni moja ya matukio mabaya zaidi kuwahi kutokea katika mji huo.

“Hili ni tukio la kusikitisha sana, pengine ni baya zaidi kuwahi kulikumba jiji letu,” amesema.