Mipango ya ATCL kumaliza hasara 2027 na tiketi za bei chee-1

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeweka mikakati madhubuti ya kubadili mwelekeo wake wa kifedha na kulifanya liachane na hasara ifikapo mwaka 2027, kutoa tiketi za bei nafuu ili kuvutia abiria wengi, huku likiendelea kupunguza ucheleweshaji na usitishaji wa safari zake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Peter Ulanga, anasema maboresho makubwa yaliyofanyika ndani ya shirika hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa yameanza kuzaa matunda, yakichochewa na ongezeko la vituo, ufanisi wa huduma na usimamizi wa karibu wa uendeshaji.

Anasema mpaka sasa ATCL ina ndege 16, ambapo 15 ni za abiria na moja ni ya mizigo, zikihudumia vituo 32 duniani kote. Kati ya vituo hivyo, 15 ni vya ndani ya Tanzania na 17 ni vya kimataifa.

Ulanga anasema ndani ya mwezi huu (Aprili) mwaka huu, shirika hilo linatarajia kufungua kituo kingine kipya, huku Mei likipanga kuanzisha safari za kwenda Seychelles, hatua itakayoongeza idadi ya vituo kufikia 34.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, tumeongeza takribani vituo nane. Hii imebadili kabisa sura ya ATCL kutoka kuwa shirika linalotegemea zaidi safari za ndani, na sasa kuwa na mtandao mpana barani Afrika, ikiwemo kufika Afrika Magharibi,” anasema.

Anaongeza kuwa shirika hilo linaendelea kutazama masoko mapya ya Kaskazini na Kusini mwa Afrika, lengo likiwa ni kupanua zaidi wigo wa biashara na kuongeza mapato ya kigeni.

Katika kuhakikisha maboresho hayo yanakuwa endelevu, Ulanga anasema timu ya juu ya uongozi imehamishia kazi zake muhimu katika jengo la Terminal One, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ili kusimamia kwa karibu mabadiliko ya shirika hilo.

Amesema makao makuu bado yapo mjini (Posta), lakini uwepo wa viongozi hao karibu na shughuli za kila siku umeongeza ufanisi katika kufanya uamuzi wa haraka na kutatua changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa safari.

“Tumekuwa na utaratibu wa wakurugenzi kuwepo kwa zamu, wakati mwingine hadi saa 12 kwa siku, wakisimamia moja kwa moja safari zote za kuondoka na kuwasili. Baada ya zamu, tunakutana na kujadili maeneo ya kuboresha,” anasema.

Mbali na hilo, anasema viongozi hao pia hushiriki safari za ndege kama abiria wa kawaida (observation flights), ili kujionea moja kwa moja ubora wa huduma na namna wateja wanavyopokelewa.

“Wanapanda ndege, wanakaa na abiria, wanaangalia utoaji wa huduma na kupata mrejesho halisi. Hii imetusaidia kufanya uamuzi unaotokana na uhalisia wa kile kinachotokea,” amesema.

Ulanga anasema maboresho hayo yameleta matokeo chanya, hasa katika kupunguza ucheleweshaji wa safari na kufuta safari bila sababu za msingi.

Anasema katika robo ya pili ya mwaka 2025 (Aprili hadi Juni), ATCL ilirekodi kufutwa kwa safari mbili pekee, huku robo ya tatu hakukuwa na safari iliyofutwa.

“Robo iliyofuata kulikuwa na visa vichache sana vya kufutwa kwa safari, na vyote vilikuwa visivyoweza kuepukika,” amesema.

Kuhusu ucheleweshaji wa safari, anasema shirika hilo linafuatilia kwa karibu kila tukio la ucheleweshaji, hata kama ni dakika moja baada ya muda uliopangwa.

“Kwa sasa tunaweza kusema zaidi ya asilimia 90 ya safari zetu zinaondoka ndani ya dakika 30 tangu muda uliopangwa. Hili ni jambo kubwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali,” anasema.

Anafafanua kuwa ucheleweshaji mkubwa unaotokea mara chache unatokana na sababu zisizoweza kuepukika, kama hitilafu za kiufundi au hali mbaya ya hewa.

“Usalama wa abiria ni kipaumbele chetu cha kwanza. Hatuwezi kulazimisha ndege iondoke ikiwa kuna hitilafu. Tutakaa, tuitengeneze au tutaibadilisha,” anasema na kusisitiza kuwa wakati mwingine safari huahirishwa au kuchelewa kutokana na hali ya hewa.

Anasema tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, kwa sasa hali ya abiria kufika uwanja wa ndege na kuambiwa safari imeahirishwa hadi kesho imepungua kwa kiwango kikubwa.

“Naamini na wewe kama ni msafiri ni shahidi kuna mabadiliko makubwa kwenye upande wa kuchelewa, kusema utafika uwanja wa ndege kisha uambiwe ndege yako leo mpaka kesho. Hizo zote ninaweza kusema mwaka 2025 na mwaka 2026 hazikuwepo,” anasema.

Anasema mradi ulioanzishwa miezi kadhaa iliyopita, unaouza tiketi hadi za Sh99,000 kwa safari kati ya Mwanza na Dar es Salaam, lengo lilikuwa ni kuhakikisha ndege zinakuwa na abiria wa kutosha, lakini pia kutoa nafasi kwa watu wenye kipato kidogo kufurahia huduma za shirika hilo.

“Shirika letu lina abiria wa aina tatu—wapo wa kibiashara, wa utalii na wengine ni wale wanaotembelea ndugu na jamaa. Wao wana uhuru wa muda wa kufanya safari muda wowote. Tukasema, kuliko ndege iende na siti tupu, ni bora watu wasafiri ndani kwa bei rahisi,” anasema.

Anasema mpango ulikuwa ni kuwawezesha watu kusafiri kwa ajili ya familia na marafiki na kurudisha imani ya Watanzania kwa kampuni yao, lakini watu wametumia fursa hiyo kwa safari za dharura wanapopata misiba na matukio mengine.

Ulanga anasema huduma hiyo imekuwa na mwitikio chanya na imepokelewa vizuri, hivyo itaendelea kutolewa kwa Watanzania. “Tunaamini huduma hii inajibu baadhi ya maeneo ambayo sisi tunaona ni jukumu letu, ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi.”

“Tunataka mtu ambaye amepata tiketi ya Sh99,000 siku moja, basi siku akiwa na pesa anunue tiketi ya kawaida. Ni jukumu letu kuiweka ATCL karibu na wananchi, ambao ipo kwa ajili ya kuwahudumia,” anasema Ulanga.

Ulanga anasema katika kipindi cha nusu mwaka 2025/2026 (Julai hadi Desemba 2025), katika hesabu ambazo hazijakaguliwa (unaudited accounts), wanaona ufanisi wa kampuni unaendelea kuimarika ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Anasema katika kipindi cha miaka hiyo mitatu, ukitoa mwaka 2025 ambapo inaonekana kama hasara imeongezeka, katika nusu mwaka ya mwaka huu kuna maendeleo makubwa na sasa shirika linajiendesha lenyewe kwa kulipa mishahara, gharama za mafuta na gharama nyinginezo.

“Maeneo ambayo Serikali imekuwa ikiwekezwa zaidi ni miundombinu, kwa maana ya majengo, hanga na, kubwa zaidi, ununuzi wa ndege. Hii ndiyo bajeti kubwa, kama ambavyo unafahamu ndege zinaponunuliwa zinawekwa kwa wakala wa Serikali,” anasema Ulanga.

Anasema mtaji wa ATCL sio mkubwa ni kama Sh16 bilioni na ununuzi wa ndege unafanywa na Wakala wa Serikali ambao ndio inanunua ndege, halafu ndege hizo kwa utaratibu uliopo zinakodishwa kwa kampuni na zikikodishwa kwa kampuni na ndiyo maana hasara inaonekana ni kubwa kwa sababu gharama za ukodishaji zinaonekana kwenye vitabu vya ATCL kama deni.

“Kwa utaratibu ule, utaona deni hilo linaongezeka na hasara inaonekana kuongezeka, lakini ukiangalia kwenye gharama za uendeshaji, je, mapato yetu yanaweza kulipia mafuta, mishahara na gharama nyingine? Jibu ni ndiyo, yanaweza, na yanazidi kuongezeka,” anasema Ulanga.

Ulanga anasema katika mwaka wa fedha uliopita (2024/2025), ulioripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hivi karibuni, kuna ongezeko la mapato la Sh143 bilioni, na kwa mwaka huu wa fedha hadi sasa wana matarajio ya ongezeko la zaidi ya Sh200 bilioni.

“Gharama kubwa zilizopo ni zile za mikataba yetu na TGFA, ikiwemo za matengenezo ya ndege. Kinachoonekana ni hasara za kihasibu, lakini kwa upande wa ufanisi wa kampuni kuna ukuaji mkubwa unaoonekana mwaka hadi mwaka,” anasema.

Kati ya mwaka 2016, wakati matarajio yanawekwa, na mwaka 2023, kuna mambo makubwa yalitokea yaliyokwamisha mipango hiyo, miongoni mwake ni Uviko-19, vita vya Urusi na Ukraine na kuharibika kwa injini za Airbus mwaka 2022/2023 (kati ya ndege nne, ilikuwa inaruka moja tu), ambavyo viliharibu mipango ya kampuni.

“Mwaka 2025 tulifanya mabadiliko makubwa, kubwa kuliko yote ni kusimamia matengenezo ya ndege zetu zote. Ilipofikia Agosti 2025, ndege zote aina ya A220 zilikuwa zinaruka, na ikawa kwa mara ya kwanza ndege zote 16 zinafanya kazi hadi sasa.

“Ni mafanikio makubwa kwa mwaka jana. Ndiyo maana utaona iliongeza hata matumizi ya kampuni, lakini faida ya kuzitengeneza hizo ndege tutaiona katika mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo mwaka huu hasara itazidi kupungua, na lengo ni kufungua maeneo mapya ya kibiashara,” anasema.

Anasema katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka huu wa fedha, kwa mara ya kwanza, safari za nje zinaingiza fedha nyingi kuliko za ndani, hivyo kuongeza mchango katika upatikanaji wa fedha za kigeni.

“Hatutegemei kuwa hadi 2027 tutakuwa bado tunapata hasara. Tuna mipango ambayo tunaipitia, na tunaangalia baada ya mwaka huu wa fedha unaoisha, kwani mabadiliko tunayoyaona huenda yakatufikisha tunapotakiwa kufika,” anasema.