Dodoma. Huenda wiki hii bungeni kukaibuka mjadala utakaohusisha mambo 10 au zaidi yanayozihusu wizara nne, ambazo mawaziri wake watasoma hotuba za bajeti mbele ya wabunge.
Wizara hizo ni Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana chini ya Joel Nanauka, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, chini ya Hamadi Masauni, Nishati, chini ya Deogratius Ndejembi na Katiba na Sheria, inayoongozwa na Dk Juma Homera.
Kwa mtazamo wa wadau, huenda mambo 10 yakawa sehemu ya hotuba za mawaziri hao. Kwa upande wa Ndejembi, hotuba yake inahusishwa na mambo kama hatua za Serikali dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta, mgawo wa umeme, kero ya maunganisho na wanaodai fidia kwa kupisha miundombinu.
Kwa upande wa hotuba ya Nanauka, inatarajiwa kugusia mikopo kwa vijana, teuzi katika vyombo vya maamuzi, elimu ya afya na maisha, huku Dk Homera akihusishwa na suala la Katiba mpya, gharama za kupata na ucheleweshaji wa kupata haki.
Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka
Kwa Masauni, hotuba yake wadau wanaihusisha kubeba mambo kama kero za Muungano, uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa, suala la hewa ukaa, mgao wa fedha za Muungano na ajira zenye usawa katika Muungano.
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamadi Masauni
Bunge limeweka siku mbili za kujadiliwa kwa hotuba ya Wizara ya Nishati, ambayo kwa nyakati hizi imebeba mambo nyeti zaidi. Hotuba za wizara nyingine zitajadiliwa kwa siku moja.
Wizara ya Nishati huenda ikabeba mjadala zaidi kwa sababu inakuja katika kipindi ambacho bei za mafuta zimepanda kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, vikihusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Kwa kuwa Serikali ilishatangaza kuwa itachukua hatua za kuwapa wananchi unafuu, hotuba ya waziri wa wizara hiyo inahusishwa na taarifa rasmi kuhusu hatua hizo zitakazowapa nafuu wananchi.
Dalili za mjadala mzito kuhusu hotuba hizo zilianza kuonekana katika michango ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wiki iliyopita. Wengi walionesha kiu ya kusubiri hotuba za wizara za kisekta.
Mbunge wa Jang’ombe (CCM), Ali Hassan King, katika mchango wake aligusia suala la mgawanyo usio wazi katika fedha za Muungano, akisema kuna shida mahali licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kero za Muungano.
Kwa upande wa mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, Kangi Lugola (Mwibara-CCM), Elibariki Kingu (Singida Magharibi) na mbunge wa Bunda Vijijini, Mwita Getere, wote walichangia kuitaka Serikali kutoka hadharani kueleza hatima ya mafuta.
Mbali na wabunge hao, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, aliibana Serikali akitaka maelezo yenye matumaini kwa Watanzania, jambo lililosababisha kuwa na mpishano wa vikao vya Kamati ya Nishati, Waziri wa Nishati, Waziri Mkuu, Spika na wataalamu.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akiwa kwenye ziara mkoani Dodoma, alizungumzia namna Serikali inavyofanya vikao vya mara kwa mara na kuahidi kuwa kila wakati watatoka hadharani kueleza hatua zinazochukuliwa ili mafuta yaendelee kuwepo kwa bei isiyo na maumivu.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi
Katika kuonesha Serikali ilivyojipanga kupunguza makali ya michango ya wabunge, mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa Bunge, Cecilia Pareso, alitangaza semina kwa wabunge itakayofanyika kabla ya wizara haijasoma hotuba yake.
“Tangazo la muhimu, waheshimiwa wabunge, Katibu wa Bunge atangaza Jumatatu ya Aprili 20 (leo) kutakuwa na semina kwa wabunge wote ili kuwapa uelewa wa suala la mafuta. Wabunge wote tunaombwa kushiriki katika ukumbi wa Pius Msekwa, na itakuwa saa saba baada ya kikao cha asubuhi,” alisema Pareso.
“Kote huko mtazunguka, lakini suala la mafuta ndiyo ajenda kuu. Ingawa naiona siku ya Jumatatu wanakwenda kutulainisha, na wala hakutatokea mvutano, badala yake utasikia hoja ya tuwaongezee fedha kwa sababu wanafanya vizuri, lakini nje wananchi watatushambulia,” amesema mmoja wa wabunge wa Viti Maalumu akiomba kuhifadhiwa jina lake.
Mbunge huyo amesema katika kipindi cha mkutano huu, moja ya wizara ambayo ingekuwa na mvutano ni nishati, na kama siyo mbinu waliyokwenda nayo, Waziri wa Nishati angekutana na moto, lakini akatabiri hoja zitasimama kwenye ukatikaji wa umeme usiokuwa na mpangilio na maunganisho, wakati suala la mafuta linaweza kuota mbawa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu, amesema kwenye Wizara ya Katiba na Sheria anatarajia kukutana na suala la Katiba mpya kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alishaahidi.
Ado amesema alianza kampeni yake kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, na alionesha mashaka kama jambo hilo litakuwepo, kwani halionekani kwenye bajeti, hoja ambayo iliwainua kundi kubwa la wabunge wakimwombea taarifa hadi kuvuruga mtiririko wa mchango wake.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dodoma, Manyanya Manyanya, amesema mkutano wa bajeti hautakuwa na maana ikiwa waziri hatakuja na hoja ya Katiba mpya.
Manyanaya amesema Katiba mpya siyo dai la Chadema wala vyama vya upinzani, bali ni hitaji la Watanzania wote, ikiwemo Chama cha Mapinduzi, na kwamba Rais Samia kwenye kampeni alishasema angeanzisha mchakato huo kwa haraka, hivyo wanangoja hiyo haraka.
“Kwanza watu watambue hizo siku 100 zimepita kama alivyoahidi kuwa angeanzia hapo. Hatuwezi kulaumu, inawezekana kuna mambo hayakuwa sawa. Leo tunakwenda na bajeti ya mwaka mzima, natamani waje na bajeti kamili ya kutuambia nini kinafanyika ndani. Watu wanataka mfumo wa kiutawala wenye uwazi, siyo hii danganya toto,” amesema Manyanya.
Waziri wa Katiba na Sheria, inayoongozwa na Dk Juma Homera
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Kata ya Mlunduzi, Mpwapwa, Julius Nhyeka, ametaka Waziri wa Vijana aje na mpango wa wazi kuhusu namna wanavyoweza kupata mikopo, akizitaja Sh200 bilioni ambazo anasema huenda zipo kwa maneno lakini si kwa uhalisia.
Julius amwsema bado kuna masharti magumu ya kuzipata fedha hizo, hasa kwenye masuala ya dhamana, ambayo wabunge wanasema yamepunguzwa, lakini uhalisia kwenye benki hauko hivyo, huku akieleza kuwa walioko vijijini ndiyo wanaweza kunufaika, lakini inakuwa vigumu watu wa benki kuwatembelea.
Hoja ya Julius imelingana na michango mingi ya wabunge, akiwemo mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Kombani, aliyeeleza Bunge kuhusu haja ya kutazama mazingira ya namna gani fedha hizo zitawafikia vijana wa vijiji, kwani kwa namna ilivyo ni kama walengwa wanakuwa wa mjini pekee.
