Kero ya barabara yaibuka bungeni, Serikali yajibu

Dar es Salaam. Serikali imeanza kufanya tathmini ya kina ya barabara zote zilizoharibiwa kufuatia mvua kubwa na mafuriko yaliyokumba maeneo mbalimbali nchini, huku ikiahidi kutoa kipaumbele kwa maeneo yaliyoathirika zaidi ili kurejesha mawasiliano ya usafiri na uchumi wa wananchi.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wabunge kuhusu ubovu wa miundombinu ya barabara, ikiwamo barabara inayounganisha Shirati Mirigo na kata ya Nyamtinga Rong’enyo katika jimbo la Rorya, ambayo kwa sasa imeharibika vibaya na kuwa vigumu kupitika.

Hoja ya ubovu wa barabara iliibuliwa tena na wabunge wakati wakichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27 ya Sh12.5 trilioni wakiitaka Serikali kuchukua hatua kwani hazipitiki hususan nyakati hizi za mvua.

Leo Jumatatu, Aprili 20, 2026, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rorya, Wambura Chege Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema Serikali imeanza kukusanya taarifa za tathmini ili kubaini kiwango cha uharibifu na gharama zinazohitajika kwa matengenezo ya haraka pamoja na mipango ya muda wa kati na mrefu.

Amesema tathmini hiyo inalenga kuhakikisha barabara hizo zinapitika haraka iwezekanavyo, huku ikiandaliwa mikakati ya kudumu ya kuzijenga kwa viwango vya juu zaidi ikiwamo changarawe na hatimaye lami kulingana na umuhimu wake.

“Tumelichukua suala hili na tunalifanyia kazi. Tumeagiza Meneja wa Tarura Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya wakamilishe tathmini haraka ili kupata gharama halisi na kuwasilisha mapendekezo Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi,” amesema Waziri huyo.

Ameongeza Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukusanya mahitaji ya fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini zilizoathiriwa na mvua, hatua itakayowezesha kutengwa kwa bajeti ya utekelezaji.

Katika hatua nyingine, Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu mpango wa ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha Kahama na mji mdogo wa Didia kupitia njia panda ya Lohumbo, katika Jimbo la Itwangi.

Akijibu swali la msingi la Mbunge, Azza Hilal Hamad, waziri huyo amesema Barabara ya Didia–Solwa yenye urefu wa kilomita 55.3 imekuwa ikipatiwa fedha kwa ajili ya ukarabati kwa miaka ya karibuni.

Amefafanua katika mwaka wa fedha 2023/2024, serikali ilitumia Sh131.78 milioni kwa ajili ya kuchonga kilomita 14, kuweka changarawe na kujenga makalavati matatu. Aidha, mwaka 2024/2025, Sh318.94 milioni zilitumika kuchonga na kuweka changarawe kilomita 13 pamoja na ujenzi wa makalavati manne.

Kwa upande wa kipande kinachoombwa kujengwa kwa kiwango cha lami chenye urefu wa kilomita 4.5, waziri amesema tayari kimeingizwa katika mipango ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kufanyiwa usanifu.

“Usanifu huo utasaidia kujua gharama halisi za ujenzi. Baada ya hapo, Serikali itaweka fedha kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi wa kipande hicho kwa kiwango cha lami,” ameeleza.

Amesisitiza Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuchochea ukuaji wa uchumi wa maeneo ya vijijini na mijini, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Hatua hizi zinatarajiwa kuleta unafuu kwa wananchi wa maeneo husika ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto za usafiri hasa wakati wa mvua, huku Serikali ikiahidi kuharakisha utekelezaji baada ya kukamilika kwa tathmini na upatikanaji wa fedha.