Na Janeth Raphael MichuziTv .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu mkubwa wa kundi la Mama na Baba Lishe nchini, akieleza kuwa ni mhimili muhimu katika kuendeleza ustawi wa jamii na uchumi wa taifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania, Rais Samia amesema kundi hilo lina mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi, wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wasafiri, wanapata huduma ya chakula kwa wakati, jambo linalosaidia kuimarisha shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa chakula ni afya, na hivyo Mama na Baba Lishe wanachangia moja kwa moja katika afya na ustawi wa wananchi, hivyo wanastahili kutambuliwa, kuheshimiwa na kulindwa katika shughuli zao za kila siku.
“Shughuli za Mama na Baba Lishe zinapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa kwa hadhi inayolingana na mchango wao katika maisha ya kila siku. Hawapaswi kusumbuliwa wala kunyanyaswa,” amesema Rais Samia.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa mazingira bora ya kisera na kisheria yatakayowezesha kutambuliwa rasmi kwa kundi hilo, pamoja na kuimarisha mchango wao katika uchumi wa taifa. Amesema hatua hiyo pia inahusisha kuimarisha sekta ya biashara ndogo ndogo kupitia mipango ya urasimishaji na uwezeshaji.
Rais Samia pia amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuweka mikakati mahususi ya kuwawezesha Mama na Baba Lishe, ili waweze kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Katika hotuba yake, alitaja pia uamuzi wa kuunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum kama moja ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha makundi mbalimbali yakiwemo Mama na Baba Lishe yanapata usimamizi na heshima stahiki.
“Serikali itahakikisha inasimamia heshima yenu na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kazi zenu muhimu kwa taifa,” alisisitiza Rais Samia.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya chakula na biashara ndogondogo, likiwa na lengo la kujadili changamoto, fursa na njia bora za kuimarisha sekta ya Mama na Baba Lishe nchini.



