Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Musoma imetupilia mbali ombi la Wambura Simbanne la kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuua bila kukusudia.
Maombi hayo yaliyowasilishwa chini ya kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura ya 141 ya mwaka 2023, mwombaji aliiomba Mahakama kumpa ruhusa ya kuwasilisha notisi hiyo nje ya muda uliowekwa kisheria, akipinga hukumu iliyotolewa Februari 22, 2022 katika kesi ya jinai namba 90 ya mwaka 2021.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya mwombaji huyo, sababu kuu ya kuchelewa ilikuwa ni kuugua, ambapo alidai aliugua baada ya kuhukumiwa na kuhamishwa kutoka Gereza la Tarime, Mkoa wa Mara hadi Gereza Kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam, ambapo aliwekwa chini ya uangalizi wa matibabu baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu.
Alidai jambo hilo lilichelewesha mawasiliano yake na ofisa uandikishaji wa gereza, ambapo kwa mujibu wa sheria alipaswa kuwasilisha notisi yake ya kukata rufaa ndani ya siku 30, ila alichelewa hadi siku 1,140 ambazo ni zaidi ya miaka mitatu.
Uamuzi huo umetolewa jana, Jumatatu Aprili 20, 2026, na Jaji Kamazima Kafanabo aliyekuwa akisikiliza maombi hayo, na nakala ya hukumu kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji amesema mwombaji huyo ameshindwa kuwasilisha sababu za msingi zinazoeleweka kisheria kuhalalisha kuchelewa kwa muda mrefu.
Katika hoja zake, Mahakama iligundua upungufu kadhaa katika kiapo cha mwombaji, ikiwemo kukosekana kwa uthibitisho wa ugonjwa alioudai, kutotajwa kwa tarehe muhimu za matukio aliyoyaeleza, pamoja na kushindwa kueleza kila kipindi cha ucheleweshaji kama inavyotakiwa kisheria.
Katika kesi hiyo ya awali, mwombaji alishtakiwa kwa kosa la mauaji, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, lakini baadaye akahukumiwa kwa kosa la mauaji bila kukusudia chini ya kifungu cha 195 cha Kanuni ya Adhabu, na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Mwombaji huyo alidai kuchelewa kwake kuwasilisha notisi ya rufaa kulitokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuugua na kuhamishwa kutoka Gereza la Tarime hadi Ukonga, hali iliyodaiwa kuathiri mawasiliano yake na mamlaka za gereza pamoja na uelewa wa taratibu za kisheria.
Mwombaji alieleza kuwa awali aliamini taratibu za kukata rufaa zilikuwa zimeanza kushughulikiwa na maafisa wa Gereza la Tarime, na kwamba hakujua kuwa notisi ya rufaa haikuwa imewasilishwa kama ilivyotakiwa.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulipinga vikali ombi hilo, ukieleza kuwa mwombaji ameshindwa kutoa sababu za kutosha kuhalalisha ucheleweshaji huo mkubwa.
Ulisisitiza kuwa sheria inamtaka mlalamikaji kuwasilisha notisi ya rufaa ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa hukumu, lakini katika kesi hiyo zaidi ya siku 1,140 zilikuwa zimepita bila hatua yoyote kuchukuliwa.
Wakili wa Serikali alieleza kuwa mwombaji hakutoa vielelezo vyovyote kuthibitisha madai yake ya kuugua, kama vile nyaraka za kitabibu, wala hakubainisha tarehe mahsusi za kuugua au kuhamishwa kwake kutoka gereza moja hadi jingine.
Mahakama, katika uchambuzi wake, ilieleza kuwa mamlaka ya kuongeza muda wa kukata rufaa ni ya hiari na hutegemea uwepo wa sababu za msingi zinazoonyesha kuwa mwombaji hakuwa na uzembe au kuchelewesha kwa makusudi.
Jaji Kafanabo alinukuu uamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufaa yanayobainisha vigezo vya kuzingatiwa katika maombi ya aina hiyo, ikiwemo urefu wa muda uliochelewa, sababu za kuchelewa, jitihada zilizofanywa na mwombaji, pamoja na uwezekano wa kuwepo hoja za msingi za kisheria katika rufaa inayotarajiwa.
Mahakama ilibainisha kuwa licha ya mwombaji kuwa mfungwa, hali hiyo peke yake haiwezi kuhalalisha ucheleweshaji wa muda mrefu kiasi hicho bila ushahidi wa kutosha.
“Ni kweli kuwa wafungwa mara nyingi wanategemea mifumo ya gereza katika kufanikisha taratibu za kisheria, lakini bado wanapaswa kuonyesha jitihada na ufuatiliaji wa karibu wa haki zao,” ilieleza Mahakama.
Mahakama pia ilisisitiza kuwa ni wajibu wa mwombaji kueleza kwa kina kila siku ya kuchelewa, hasa pale ambapo muda uliopita ni mrefu, ili Mahakama iweze kutathmini uhalali wa sababu zinazotolewa.
Katika uamuzi wake, Mahakama ilinukuu msimamo wa muda mrefu wa mahakama kwamba, ingawa huruma inaweza kuzingatiwa katika baadhi ya mazingira, haiwezi kuchukua nafasi ya misingi ya kisheria pale ambapo hakuna sababu ya msingi iliyoonyeshwa.
“Mahakama haipaswi kuongozwa na huruma pekee iwapo hakuna udhuru halali unaothibitishwa. Haki lazima itendeke kwa kuzingatia sheria,” ilieleza hukumu hiyo.
Kwa kuzingatia hoja zote zilizowasilishwa, Mahakama ilifikia hitimisho kuwa mwombaji ameshindwa kuonyesha sababu za kutosha za kucheleweshwa kwake kwa zaidi ya miaka mitatu na miezi saba. Kutokana na hali hiyo, Mahakama iliamua kuwa ombi hilo halina msingi wa kisheria na hivyo kulikataa.
