Dar es Salaam. Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), imeliomba Bunge kuidhinishia Sh76.68 bilioni ili kutekeleza vipaumbele vitano kikiwemo cha kuimarisha Muungano kwa mwaka 2026/27.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni vipaumbele vingine, hifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Vingine ni uratibu wa shughuli za uchumi wa buluu, kuratibu utekelezaji wa miradi na shughuli za wezeshi za hifadhi na usimamizi wa mazingira na kazi nyingine zitakazotekelezwa na ofisi hiyo.
Waziri Masauni ameomba fedha hizo leo Jumanne Aprili 21, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma.
Amesema kwa fedha wa 2026/27 ofisi hiyo imepanga kuendelea na utekelezaji wa mpango kabambe wa elimu kwa umma kuhusu Muungano utakaohusisha maandalizi ya ujenzi wa vituo vya kumbukumbu na nyaraka za Muungano.
“Kuendeleza tafiti kuhusu uelewa wa vijana katika masuala ya Muungano Tanzania Bara na Zanzibar, kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo zinazotekelezwa pande mbili za Muungano,”
“Kuratibu vikao vya kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kushughulikia Muungano ikiwemo kukamilisha utatuzi wa hoja za kuhamasisha fursa za Muungano,” ameeleza Masauni.
Masauni amesema Serikali imepanga kuratibu utekelezaji wa Dira ya 2050 katika masuala yanayohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Katika kufanikisha hilo, kutafanyika utekelezaji wa programu ya mageuzi ya kimkakati ya mazingira endelevu Tanzania ili kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 19.
Masauni amesema ofisi hiyo itaendelea kuimarisha mfumo wa uratibu wa shughuli za uchumi wa buluu kwa kuandaa mwongozo wa uratibu pamoja na kuandaa mpango kabambe wa uwekezaji katika sekta za uchumi wa buluu.
Mbali na hilo, Masauni amesema itaandaa mpango na bajeti ya Ofisi na taarifa za utekelezaji wa mipango mbalimbali ikiwemo kuelimisha umma kuhusu majukumu, sera, mikakati na programu zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Waziri Masauni amesema Serikali imepanga kutekeleza mradi wa kujenga ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi mkoani Kigoma
Mradi mwingine ni kuimarisha jamii na mifumo ikolojia katika kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye ukanda wa misitu ya miombo wa Tanzania Bara na maeneo kame ya Zanzibar.
