Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matano yanayolenga kuboresha sekta ya mama na baba lishe nchini, akisisitiza kuwa kundi hilo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kila siku na ustawi wa jamii.
Maagizo hayo ameyatoa leo Jumanne, Aprili 21, 2026, aliposhiriki kongamano la mama na baba lishe lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kundi hilo liendelee kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa.
Rais Samia ametoa maagizo hayo akizilenga wizara, taasisi na mamlaka mbalimbali kuhakikisha changamoto zinazolikabili kundi hilo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu, huku akikemea manyanyaso yanayofanywa hususan na mgambo.
Rais Samia ameagiza kuboreshwa kwa miundombinu ya masoko na maeneo ya biashara kwa mama na baba lishe nchini, akiwataka viongozi wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wakuu wa mikoa na wilaya kushirikiana kuhakikisha wanatenga maeneo rasmi yenye huduma muhimu kwa ajili ya kundi hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa amevaa sare za Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) mara baada ya kukabidhi mitungi ya gesi na majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, Aprili 21, 2026.
Amesema maeneo hayo yanapaswa kuwa na mazingira safi na salama yatakayowezesha wafanyabiashara hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Pili, ameagiza utoaji wa mafunzo maalumu ya kidijitali kwa mama na baba lishe ili watumie teknolojia katika kukuza biashara zao. Hii ni pamoja na matumizi ya programu ya Umalita App, ambayo amesema inaweza kuwa fursa kubwa ya kuwainua kiuchumi iwapo watapatiwa ujuzi wa kuitumia ipasavyo.
“Waziri (Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki), nenda kawatimizie haja yao wapate mafunzo ili waitumie vizuri na kuwasiliana kwa urahisi,” ameagiza Rais Samia.
Tatu, Rais amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kifedha na kijamii, akitaja mikopo nafuu, bima ya afya na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa ni mahitaji muhimu kwa kundi hilo.
Ameagiza taasisi husika, ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kufika moja kwa moja kwa mama na baba lishe ili kuwapa elimu na kuwawezesha kujiunga na huduma hizo.
Nne, ameelekeza kuimarishwa kwa matumizi ya nishati safi katika shughuli za upishi ili kulinda afya za wafanyabiashara hao pamoja na mazingira. Amesema mageuzi ya matumizi ya nishati ni sehemu ya mabadiliko ya kimtazamo na kiteknolojia yanayopaswa kuungwa mkono na wadau wote.
“Tumeambiwa ladha ya chakula haibadiliki, hivyo ni wakati wa kufanya mageuzi haya kwa manufaa ya afya na mazingira,” amesisitiza.
Tano, Rais Samia ametoa agizo la kuanzishwa kwa vituo vya malezi ya watoto katika maeneo ya biashara ya mama lishe ili kuwawezesha kufanya kazi zao bila wasiwasi. Amesema suala hilo ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora huku wazazi wao wakifanya shughuli za kiuchumi.
Mbali na maagizo hayo, Rais Samia pia ametambua mchango mkubwa wa mama na baba lishe katika kulisha Taifa, akisema kundi hilo linawezesha utekelezaji mzuri wa shughuli za kila siku za kiuchumi.
“Ninyi ni kundi muhimu sana katika jamii, mnalisha wafanyakazi na wananchi kwa ujumla na hivyo kuwezesha shughuli za nchi kuendelea kila siku,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa ajili ya kundi hilo, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa wizara inayoshughulikia maendeleo ya jamii na makundi maalumu.
Changamoto na ahadi ya kuzitatua
Akizungumzia changamoto zinazowakabili, Rais Samia amesema Serikali inazitambua na itazifanyia kazi. Baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa mitaji, maeneo rasmi ya biashara pamoja na huduma za kijamii.
Aidha, ameahidi kuwa mlezi wa kundi hilo hata baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi, akisisitiza dhamira yake ni kuhakikisha wanapata heshima na kutambuliwa wanavyostahili.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amesema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha ustawi wa makundi maalumu, ikiwemo mama na baba lishe, akibainisha kuwa hoja zao zimekuwa zikipewa uzito mkubwa hata katika kamati za Bunge.
Amesema wakati wa mijadala bungeni, masuala ya makundi hayo yamekuwa yakihojiwa kwa kina, na Serikali imeeleza mikakati mbalimbali itakayoboresha mazingira yao ya kiuchumi na kijamii.
Katika kongamano hilo, Rais Samia alikabidhi hundi ya Sh94.1 bilioni kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, ikiwa ni fedha kwa niaba ya wafanyabiashara ndogondogo, wakiwemo mama na baba lishe, ili kuwawezesha kukuza biashara zao.
Pia, Rais Samia alipewa tuzo ya “Malkia wa nishati safi” iliyotolewa na Chama cha Mama na Baba Lishe Tanzania (Umalita), kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hatua inayolenga kuboresha afya na mazingira ya wafanyabiashara hao nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk John Jingu, amesema kongamano hilo limekusudiwa kuwa jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mustakabali bora wa sekta ya mama na baba lishe nchini.
Amesema kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa, washiriki wamepata fursa ya kujadili namna ya kuboresha huduma zao huku wakizingatia afya, usalama wa chakula na utunzaji wa mazingira.
Katibu Mkuu wa Umalita, Julieth Madata, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa kundi hilo, akiwapa nguvu ya uthubutu wa kujenga na kukuza biashara zao hata katika mazingira magumu.
Madata amesema kupitia sera na miongozo ya Rais Samia, mama na baba lishe wamepata hamasa mpya ya kujikwamua kiuchumi, huku akieleza kuwa uongozi wake umeweka mazingira rafiki ya kuwainua wanawake na makundi ya kipato cha chini.
“Nafasi yake kama Mama wa Taifa imekuwa nguzo muhimu kwetu; ametuwezesha kuona kuwa inawezekana kuinuka kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa moja ya mafanikio makubwa ni kuhamasishwa kwa matumizi ya nishati safi badala ya kuni na mkaa, hatua ambayo imeboresha mazingira ya kazi na afya za wafanyabiashara hao.
Amesema hadi sasa Umalita ina wanachama zaidi ya 5,000 nchini, ambapo 1,600 wapo Dar es Salaam pekee, huku wakilenga kufikia wanachama 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, ameeleza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa huduma za hifadhi ya jamii, uhaba wa vizimba pamoja na kukosa masoko ya kudumu.
Madata amesisitiza kuwa mama na baba lishe ni mhimili muhimu wa jamii, kwani huhudumia sehemu kubwa ya wafanyakazi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla, hivyo kuna haja ya kuweka mazingira bora zaidi yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi.
Pamoja na hayo, amezitaja changamoto zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa huduma za hifadhi ya jamii, kukosa vizimba na masoko pamoja na kusumbuliwa na kundi la askari mgambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na makundi ya mama na baba lishe nchini kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kukuza biashara zao kutoka ngazi ndogo hadi kuwa endelevu.
Mwambapa amesema CRDB Bank Foundation imejikita katika kukuza ujumuishi wa kifedha kwa kutoa mitaji wezeshi kwa makundi maalumu. Amesema hadi sasa wamefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh6.7 bilioni kwa riba nafuu ya asilimia 10, huku marejesho yake yakiwa ya kuridhisha.
Mwambapa ameeleza kuwa miongoni mwa wanufaika wakuu wa mikopo hiyo ni mama na baba lishe, ambao wameendelea kuonyesha nidhamu nzuri ya fedha na uwezo wa kukuza biashara zao.
Ameongeza kuwa CRDB Bank Foundation pia inawekeza katika vijana na ubunifu, akipongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mikakati inayolenga maendeleo ya vijana. Amesema kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali, ikiwemo COSTECH, vijana wanawezeshwa kubadilisha biashara zao kuwa makampuni na hivyo kuongeza ajira.
Aidha, kupitia programu za IMBEJU na taasisi za wanawake, zaidi ya wanawake 10,000 wamefikiwa kwa elimu ya ujasiriamali na mitaji, hatua inayochochea uwezeshaji wa kiuchumi na utunzaji wa mazingira.
Kaulimbiu ya kongamano hilo imejikita katika kuhimiza amani na mshikamano wa Taifa, huku ikisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta zote, ikiwemo biashara ndogondogo za mama na baba lishe.
