Ulega aipa Tanroads siku 14 kumpata mkandarasi barabara ya Kisarawe–Maneromango

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kisarawe hadi Meneromango, mkoani Pwani.

Katika mchakato huo, Waziri Ulega ameitaka Tanroads kuona umuhimu wa kuharakisha utekelezaji huo bila kukiuka taratibu za kisheria.

Ulega ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Aprili 21, 2026, akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masaki, Kisarawe, akieleza kuwa ndani ya wiki mbili mkandarasi huyo atapatikana ili kuanza mradi huo.

“Wana Masaki, leo kazi yangu ni moja tu, kuiagiza Tanroads kukamilisha taratibu zote za kitaalamu ili ujenzi uanze.

“Matumaini yangu mmeshakamilisha taratibu zenu za ndani, hivyo ndani ya wiki mbili nahitaji kufahamu ni mkandarasi gani amekidhi vigezo ili aanze kazi,” amesisitiza Ulega.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma zote muhimu za kijamii, zikiwemo elimu, afya, miundombinu na kilimo, hatua itakayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Waziri Ulega amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ya barabara, ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja.

Katika hatua nyingine, Ulega amerejea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu barabara zote mpya kuwekwa taa, ili kuongeza usalama na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika muda wote.

Pia ameagiza kushughulikiwa kwa barabara iliyokatika katika eneo la Vikumburu, akitaka wahusika kurejesha mawasiliano haraka na kuweka kambi ya muda ili kazi hiyo ifanyike mchana na usiku hadi itakapokamilika.

Kuhusu ombi la mbunge wa Kisarawe, Dk Suleiman Jaffo, la uharibifu wa barabara ya Dondwe–Lukwali hadi Njia Nne, Ulega ameagiza wataalamu kufika mara moja eneo hilo na kuanza matengenezo.

Kwa upande wake, Dk Jaffo amesema hali ya miundombinu imekuwa changamoto kubwa, akieleza kuwa baadhi ya mabasi yamelazimika kusimama kwa muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara.

Mkazi wa Kisarawe, Madebe Lidai, ameeleza kuridhishwa na mradi huo, akisema utaleta mageuzi makubwa katika usafiri na uchumi wa eneo hilo.

“Tunashukuru, kwa kuwa hii barabara yenye urefu wa kilomita 34.5 kutoka hapa Sungwi hadi Maneromango itatusaidia vyombo vya usafiri kuwa salama na kufika kwa haraka zaidi,” amesema Madebe.

Barabara hiyo inaunganisha maeneo muhimu yakiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, Hifadhi ya Selous na Mloka wilayani Rufiji, hivyo itachochea shughuli za biashara na uwekezaji katika ukanda huo.