Muuguzi adaiwa kuuawa na mpenzi aliyemsomesha kisa wivu wa mapenzi

Same. Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Mji Same mkoani Kilimanjaro, Asha Bakari (25), anadaiwa kuuawa kwa kukatwa shingo na mpenzi wake, huku chanzo cha tukio hilo kikihusishwa na wivu wa mapenzi.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 21, 2026, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Mgeni amesema tukio limetokea jana Jumatatu, Aprili 20, 2026, katika Kata ya Kisima, karibu na hospitali hiyo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, amesema mauaji hayo yalitokea saa tatu usiku.

Amesema Asha alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea hospitalini hapo na alishambuliwa akiwa nyumbani kwake.

“Mtumishi wa Hospitali ya Mji Same aliuawa kwa kuchomwa kisu na mpenzi wake katika eneo la makazi karibu na hospitali aliyokuwa akifanya kazi,” amesema Mgeni.

Ameongeza kuwa kabla ya kutokea kwa mauaji hayo, alipigiwa simu na mtuhumiwa akimtaka wakutane, ndipo alipofika nyumbani kwake na kutekeleza mauaji hayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu huyo, marehemu alikuwa na uhusiano na wanaume wawili, lakini mmoja wao na ndiye aliyemsaidia kumsomesha hadi kufikia hatua ya kupata ajira.

“Inadaiwa kuwa baada ya kuanza kazi alianza  uhusiano mwingine na mtumishi wa hospitali hiyo, jambo lililomkera mtuhumiwa na kusababisha kutokea kwa tukio hili la kikatili,” amedai mkuu huyo wa wilaya akirejea taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi wilayani Same.

Mgeni amesema baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye ni dereva wa bodaboda alitoroka na kutokomea kusikojulikana, huku juhudi za kumsaka  zikiendelea.

“Tayari tumemtambua kwa jina na kazi yake. Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka, akipatikana atafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Amesema muuguzi huyo alifariki dunia muda mfupi baada ya kushambuliwa kwa kuchomwa kisu shingoni.

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kisima, Kei Mbwambo amesema ni tukio la kinyama na kifo hicho ni pigo kwa wakazi wa eneo hilo kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ameanza kazi ya kuwahudumia.

“Hili ni tukio la kusikitisha na la kikatili. Haikubaliki kwa mtu kuchukua uhai wa mwingine kwa namna hii, hata kama kulikuwa na tofauti zozote za kimahusiano,” amesema Mbwambo.