Frantz Fanon, alikuwa mtaalamu magonjwa ya akili. Asili yake ilikuwa Ufaransa na Visiwa vya West Indies (Caribbean). Fanon, pia alikuwa Marxist, yaani mfuasi wa gwiji wa falsafa za kisiasa, hasa za mrengo wa kushoto, Karl Marx.
Katika maandiko yake, Fanon alieleza kwa upana kuwa athari za ukoloni kwa sehemu kubwa ni jamii zolizotawaliwa kuuacha utamaduni na desturi zao, kisha kukumbatia ‘fasheni’ za wageni waliowatawala. Fanon alisema, wakoloni waliacha athari ya ugonjwa wa akili katika maeneo waliyoyakalia.
Katika kufafanua, Fanon alisema ugonjwa wa akili ambao umesababishwa na ukoloni ni matatizo ya kisaikolojia yenye kwenda sambamba na kupuuza lugha za ndani na kutukuza za kigeni, kudharau urithi wao na kushabikia “uzungu”. Kupuuza misingi yote ya asili na kukumbatia yale yenye kutoka kwa wakoloni.
Fanon alikwenda mbele ya Muitaliano, Antonio Gramsci, ambaye naye ni Marxist. Gramsci alitambulisha nadharia inayoitwa “Cultural Hegemony,” yaani utamaduni wa nchi au bara moja kuongoza dunia. Mathalan, hivi sasa, utamaduni wa kisiasa na uongozi unaopigiwa chapuo ni ule wa Magharibi.
Mataifa ya Afrika na Latini America (Global South), yanachukua muundo wa siasa, yananakili Katiba za nchi za Magharibi, kwa kuona kwamba aina ya utawala wa Marekani na Ulaya Magharibi ndiyo sahihi.
Na hii ndiyo ambayo mwanazuoni wa Iran, Jalal al-e Ahmad, aliita “Gharbzadegi”, ambalo ni neno katika lugha ya Kiajemi, likiwa na maana ya kupotea kwa utamaduni wa kiasili kwa upofu wa kuona Wazungu ni bora.
Nadharia ya Gharbzadegi hutumika kuchambua jinsi Iran inavyotafsiriwa na nchi za Magharibi kama taifa lenye misingi ya kidikteta, kwamba wanawake wananyanyaswa, kwa sababu ya imani kuwa mifumo ya Ulaya na Marekani ndiyo kipimo cha ulimwengu.
Wakati huohuo, Serikali ya Mapinduzi Iran, inatembea na mtazamo kuwa misingi yao ndiyo ustaarabu wa dunia unapaswa kuwa.
Ufafanuzi unaweza kuwa mrefu lakini mantiki ni kwenda pamoja na mada ninayoilenga. Nchi inazungumza maridhiano, je, tunayafikiaje? Tunaweza kufanikiwa kwa kutembea na mitazamo kuwa tunapogombana, nchi za Magharibi zitaingilia kati? Je, kwa kuamini kwamba Tanzania ni yetu, na lazima matatizo yetu tuyatatue kama Watanzania?
Tunaweza kufikia maridhiano tukiwa na hisia kuwa tusipofikia makubaliano tutaitisha jumuiya za kimataifa ziiwekee vikwazo Tanzania? Haya ni mawazo ya ugonjwa wa ukoloni.
Tanzania ni nchi huru, inayoongozwa na Watanzania. Inatakiwa mazungumzo yafanyike kwa kutambua kwamba maridhiano yenye tija kwa nchi ndiyo mwafaka kwa maendeleo ya taifa.
Je, maridhiano yatapatikana kwa imani kuwa wakisusa maridhiano watapelekwa jela kwa kesi za uchochezi au uhaini? Au watadhibitiwa kufanya siasa? Hapana, mitazamo ya namna hiyo pia ni batili. Ugonjwa wa ukoloni una matawi mawili, kushabikia Wazungu kama majuha, lakini tawi la pili ni kukandamiza ndugu zako kwa sababu una nguvu au ndiye umeshika mamlaka.
Maridhiano ya kitaifa yapatikane baada ya tafakuri ya kina, ambayo itazileta pande zote kwenye dirisha la kukiri makosa na kujisahihisha. Kukumbuka kuwa kuna watu walipoteza maisha. Kutambua uzembe na ujuaji wa pande zote. Kuheshimiana kwenye meza ya mazungumzo. Kusikilizana na kuelewa hoja za pande zote.
Haiwezekani kupata mwafaka utakaojenga maridhiano kama kuna wanaomini wao ni Watanzania sana kuliko wenzao. Wanaoona utanzania wao ni kipeo cha pili, na wengine hawana uraia kamili.
Kuingia kwenye mazungumzo ya maridhiano ukiwa na madai ya Tanganyika inatawaliwa na Wazanzibari, ni sawa na kusema hutaki maridhiano.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dola iliyoundwa na Watanzania wenyewe. Tanganyika na Zanzibar ni mipaka iliyowekwa na Wakoloni. Unaweza kujiuliza, je, busara za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, hazina maana mbele ya mipaka ya Wakoloni? Kuelekea meza ya mazungumzo ni vizuri mno kuukataa ugonjwa wa ukoloni.
Maridhiano yabebe malengo ya kuilinda Tanzania na kuipa hadhi kwenye uso wa dunia. Ionekane kuwa Watanzania kutofautiana si jambo la ajabu, lakini nyakati zote, baada ya tofauti zao, huketi pamoja na kuelewana, kisha kusonga mbele.
Ndivyo iliwezekana baada ya ghasia za Januari 26 na 27, 2001, Pemba, Unguja na Dar es Salaam. Ikawezakana baada ya mauaji ya kisiasa Arusha mwaka 2011.
Kutambua na kuheshimu viongozi waliopo kutarahisisha mazungumzo na kuielekea suluhu. Kuwakataa kutafanya mazungumzo yasiwezekane. Hoja za maridhiano zinapaswa kujikita katika kuinasua nchi mahali ilipo ili kuiendea kesho yenye neema, bashasha na upendo kwa wote. Makosa yaliyotokea yanapaswa kutazamwa ili maridhiano yawe na maana.
Kukwama kwenye makosa yaliyotokea. Kutumia muda mrefu kulaumiana. Kusutana vikaoni na kuhukumiana, hakutaleta ufumbuzi. Nchi inatakiwa iwe moja.
Uchochezi wa nje uonekane kwa kila upande. Lugha mbaya kwa viongozi itambulike na iwaudhi wote. Huwezi kuingia kwenye maridhiano na watu ambao wanalea makundi ya vijana wanaotukana viongozi mitandaoni.
Tanzania ni ya Watanzania. Mariadhiano yawe na shabaha ya kuwafanya watanzania wote waione nchi yao kuwa mahali salama pa kuishi. Kusiwepo wenye fikra za kunufaika binafsi au kikundi chao.
Kusiwe na wenye agenda zilizokolezwa wino nje ya mipaka. Vikaoni, wajumbe watazamane kama ndugu wenye malengo ya kujenga nyumba yao iliyo bora.
Lugha za ubaguzi ni matokeo ya athari za ukoloni. Mikutano izungumze kitanzania kwa ajili ya utanzania, Tanzania na Watanzania. Ubishani wa kisiasa haupaswi kupewa nafasi, badala yake hoja zijikite kwenye kuwafanya watoto wa makundi rika ya vijana wa sasa (Generation Y “Millennials” Z na Alpha), wawe na taifa bora kabisa. Yaani, kuijenga kesho na kushokutwa yenye manufaa na vizazi vya sasa na vinavyokuja.
