YANGA inapiga hesabu mpya juu ya kuboresha ukuta wake na wakati wowote inaweza kumng’oa beki wa kazi pale TRA United.
Dili la kifaa hicho kipya, linatishia nafasi ya beki Mghana, Frank Assinki ambaye anacheza kwenye kikosi hicho cha Yanga kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.
Iko hivi; Yanga imekubali uwezo wa beki Nasry Kombo ambaye ni nahodha wa TRA United wakati akiwazuia washambuliaji wa kikosi hicho, kisha Simba kwenye mechi mbili tofauti za Ligi Kuu Bara zilizochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, hivi karibuni.
Yanga baada ya kuona uwezo wa nahodha huyo, inapiga hesabu za kumalizana naye mapema ili aende kuongeza nguvu kwenye ukuta wa kikosi hicho kwa msimu ujao, huku ikitaka kuwa na mabeki wa kati wote wazawa, ikipiga hesabu za kupunguza wachezaji wa kigeni.
Endapo Yanga ikimpata Kombo, imepanga kutoendelea kuwa na Assinki, hivyo atarudi Singida Black Stars.
Katika uamuzi huo, Yanga inataka kutumia nafasi ya Assinki kuongeza mashine nyingine kwa wachezaji wa kigeni katika maeneo ya kiungo ambako ndiko inataka kuifanyia marekebisho makubwa kwa msimu ujao.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti: “Kuna yule Kombo ambaye yupo TRA, ni beki mzuri sana, ameonyesha kiwango bora sana msimu huu, kama mambo yatakwenda vizuri tutamchukua, tumeshaanza naye mazungumzo kama tukikubaliana tutakuwa naye.
“Kama tukimpata hatutakuwa na sababu ya kuendelea na Assinki, ni beki mzuri lakini hesabu zetu ni umakini kwenye hawa wachezaji wa kigeni, tutatumia nafasi yake kutafuta kiungo mmoja wa kimataifa ambaye tunamtaka aje msimu ujao.”
Kombo alipokutana na Yanga kisha Simba wakati TRA United ikiwa nyumbani Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, beki huyo alicheza mechi zote hizo za Ligi Kuu Bara akilinda vizuri lango lao ambalo nyavu zake hazikutikiswa, matokeo yakiwa 0-0.
Lakini beki huyo hakuwa na bahati Machi 22, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar, pale TRA United ilipofungwa mabao 3-0 na Simba katika ligi, huku yeye akiwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo. Ndani ya kikosi cha TRA United, Kombo anacheza pacha na Chamou Karaboue.
Habari njema kwa Yanga ni kwamba, mkataba wa Kombo na TRA United unamalizika mwisho wa msimu huu ingawa mabosi wa klabu yake wanataka kumuongezea mkataba mpya kufuatia jina lake kupitishwa na kocha Ettiene Ndayiragije kwa nyota wanaohitajika kuendelea kusalia kikosini hapo.
Katika kikosi hicho, mabeki wa kati hivi sasa ni nahodha Bakari Mwamnyeto, msaidizi wake Dickson Job, Ibrahim Bacca na Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ ambao wazawa, huku Assinki akiwa pekee wa kigeni.
