Che Malone afichua jambo Simba fainali ya CAF

BEKI wa kati wa USM Alger na timu ya taifa ya Cameroon, Che Malone Fondoh ameitaja Simba kuwa na nafasi katika safari yake ya mafanikio Afrika, baada ya kutinga fainali ya pili mfululizo katika Kombe la Shirikisho.

Che Malone alisema uzoefu alioupata akiwa Simba ndani ya miaka miwili, ulimjenga na kumuweka katika kiwango cha juu cha mashindano ya CAF, jambo lililomsaidia hata akiwa na USM Alger msimu huu.

“Simba ni sehemu ya historia yangu. Nakumbuka vizuri vile ambavyo tulikuwa katika nafasi ya kufanya kitu lakini ndio mpira ulivyo na maisha lazima yaendelee kwangu, hii ni nafasi nyingine ya kupigania taji,” alisema.

Akiwa na Simba, Che Malone alicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na Wekundu wa Msimbazi walipoteza dhidi ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1. Katika fainali hiyo msimu uliopita 2024-2025, ilichapwa 2-0 ugenini na kutoa sare ya 1-1 nyumbani.

Msimu huu, beki huyo ameendeleza kiwango chake akiwa na USM Alger, ambapo amefanikiwa tena kufika fainali ya michuano hiyo baada ya kikosi hicho kuitoa Olympique Safi kwenye hatua ya nusu fainali.

USM Alger sasa itakutana na Zamalek ya Misri kwenye fainali, huku Che Malone akiwa na nafasi ya kucheza fainali yake ya pili mfululizo katika michuano hiyo mikubwa ya CAF kutokana na kiwango chake bora.

Katika msimu huu, Che Malone ameichezea USM Alger mechi 12 sawa na dakika 1,080 katika Kombe la Shirikisho Afrika na kufunga bao moja hatua ya makundi dhidi ya FC San Pedro ya Ivory Coast, licha ya nafasi yake kuwa ni beki wa kati.

Msimu uliopita akiwa Simba, alicheza mechi tisa ndani ya dakika 758, akiwa sehemu muhimu ya kikosi kilichoandika historia ya kufika fainali ya CAF kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 32.

Tangu ajiunge na USM Alger, Che Malone pia amekuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon, ambapo ameshiriki michuano mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) zilizofanyika Morocco, ambapo Cameroon ilifika hatua ya robo fainali.