Makalla amzawadia Chobwedo njumu, amtaka kuendelea kupambana

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla leo Jumanne Aprili 21, 2026 amekutana na kumpatia zawadi ya viatu winga wa TRA United, Ramadhan Salum “’Chobwedo’, akimsifu kwa kiwango kizuri alichokionesha katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC.

Makalla ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo, yenye makazi yake Arusha, amesema Chobwedo ameonesha kiwango kizuri kwenye mechi za TRA dhidi ya Yanga, mbili za Simba dhidi ya zilizochezwa Dar Es salaam na Arusha pamoja na mechi dhidi Pamba, akimtaka pia kuwa makini na mitandao ya kijamii na asikubali ikawa sehemu ya kumvunja moyo kutokana na ukosoaji kadhaa wa watumiaji wa mitandao unaoelekezwa kwa mchezaji huyo.

“Mimi nimecheza mpira katika kiwango kikubwa lakini pia nimefundisha kwahiyo nikikupa sifa nakupa sifa za ukweli na nikisema hii ni mali basi ni mali kweli, wewe Chobwedo ni mali”.

Nimefuatilia mechi zenu nikiwa huko nje ya nchi (Uturuki) nikasema nikuletee zawadi tena ya ‘bei mbaya’ (Kiatu chapa ya NIKE) na bei yake ni Dola 400 za Marekani ambayo ni zaidi ya Sh 1 milioni za kitanzania, nikutakie kila la kheri na mimi nakutia moyo nenda kapambane.” amesema Makalla.

Kwa upande wake Chobwedo, amemshukuru Makalla kwa malezi yake kwa timu hiyo tangu ilipohamia mkoani Arusha kutoka Dar es Salaam, akimshukuru pia kwa zawadi aliyompatia na kumuombea kheri .

Chobwedo amekuwa gumzo msimu huu akionyesha kiwango kikubwa akiwa na TRA United, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo (Man of the Match) mara tatu, akifanya kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga na Singida Big Stars.