KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, amezichimba mkwara timu tatu kubwa Simba, Yanga na Singida Black Stars akisema hawezi kukubali timu hiyo kuendelea kugeuka ngazi ya mafanikio.
Azam leo itaanza mashindano ya Kombe la Muungano ikiikaribisha KVZ yenye mastaa wawili waliocheza Ligi Kuu Bara, Sixtus sabilo na Kelvin Kongwe Sabato, mchezo utakaopigwa Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani hapa kuanzia saa 1:15 usiku.
Mara ya mwisho Azam kutinga fainali ya Muungano ilikuwa 2024 lakini ikakubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Simba lakini pia Ibenge alikuwa hapa Zanzibar Januari 2026, akiiongoza Azam kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa kisiwani Pemba matajiri hao wakapoteza kwa matuta dhidi ya Yanga.
Hatua hiyo ndio imemuibua Ibenge akisema safari hii kikosi chake hakitaki kufanya makosa yaliyofanyika nyuma ambapo kila mchezo wataubeba kama fainali ili kushinda.
Ibenge alisema Azam inalitaka Kombe la Muungano ambapo haitajali inakutana na timu ipi, akisema wanaheshimu ubora wa kila kikosi watakachokutana nacho kuanzia hatua ya mtoano mpaka fainali.
“Tumeshakuja hapa Zanzibar mara mbili lakini tumeshindwa kupata kombe mara zote timu ikifika mpaka fainali, tunajua kila timu ni bora, unaposhindana na timu kama Simba, Yanga na Singida unatakiwa kuwa bora na sisi ni bora tunataka kushinda safari hii,” alisema Ibenge.
“Kila mchezaji tumekuja naye hapa, tutacheza kwa malengo ya timu inayotaka ubingwa, Azam ni timu kubwa haitakiwi kuendelea kuwa nyuma ya timu zingine zikipata mafanikio.”
Msimu huu Azam haijapoteza mchezo wowote mbele ya Simba, Yanga wala Singida katika Ligi Kuu Bara ambapo rekodi hiyo imemfanya Ibenge kutamba kwamba kikosi chake kinahitaji heshima ya kupata taji la Muungano.
“Kila timu inatamani kushinda mbele ya timu hizi kubwa, sisi tumeshinda michezo mwili na kukitoa sare tatu, hii ina maana kwamba tunaweza kufanya kitu tofauti ndio maana tunautaka ubingwa.”
KVZ vs Azam (Saa 1:15 Usiku)
Mlandege vs Singida BS (Saa 10:15 Jioni)
Simba vs Mafunzo (Saa 2:15 Usiku)
