TANZANIA NDANI YA 10 BORA UTOAJI WA TAARIFA WTO

Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za juu katika utoaji wa taarifa za biashara kati ya nchi 166 ambazo ziko chini ya Shirika la Biashara Duniani (WTO).

Hayo yamesemwa na na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Needpeace Wambuya wakati akifungua Warsha ya kitaifa ya mafunzo kuhusu taarifa za Shirika la Biashara Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Aprili 21, 2026 katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Bw. Wambuya amesema mafunzo hayo yatasaidia kuvutia wawekezaji, kuwa na imani na taarifa, kuongeza uwazi wa taarifa na kufanya taarifa zinazopelekwa zisaidie kuondoa vikwazo vya kibiashara ambazo zimekuwa ni changamoto ya ufanyaji wa biashara duniani.

Amebainisha kuwa mafunzo hayo yamewalenga wataalam wa sekta za Serikali lakini na sekta binafsi kwa nia ya kuwajengea uwezo wataalamu wa biashara juu ya namna ya kuratibu utoaji wa taarifa aina ya taarifa za biashara zinazotolewa na wakati unaofaa kutoa taarifa.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku nne katika Ofisi za Wizara ya Viwanda na Biashara yakijumuisha maafisa kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.