Aliyemuua mumewe akiwa na hawara ahukumiwa kifungo cha nje

Songwe. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songwe, imemhukumu kifungo cha nje cha miezi 18, Elizabeth Sylvester maarufu Sosomo, mkazi wa Kijiji cha Chudeko, Wilaya ya Songwe, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mumewe, Ally Masanja bila kukusudia.

Katika kesi namba 7304/2026 iliyosikilizwa na mahakama hiyo, mshtakiwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Elbariki Mpinga, tukio hilo lilitokea Januari 3, 2026 katika Kijiji cha Chudeko, wilayani Songwe mkoani Songwe. Ilielezwa kuwa mshtakiwa alimchoma mumewe kisu ubavuni wakati wa ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa ugomvi huo ulizuka baada ya mshtakiwa kumkuta marehemu akiwa katika nyumba ya mwanamke mwingine anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye. Tukio hilo lilisababisha mzozo kati ya wahusika hao watatu na kuishia katika shambulio lililosababisha kifo cha marehemu.

Akisoma hukumu hiyo jana Jumanne, Aprili 21, 2026, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Gabriel Malata alisema mahakama imezingatia mazingira ya tukio hilo, ikiwemo hali ya mshtakiwa kabla, wakati na baada ya tukio pamoja na kukiri kwake kosa hilo.

Alisema kutokana na vigezo hivyo, mahakama imemtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya vifungu husika vya sheria na kuamua kumpa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi 18 badala ya kifungo cha gerezani.

“Hivyo, mahakama inaamuru mshtakiwa kutumikia kifungo cha miezi 18 nje ya gereza kwa kuzingatia masharti yote ya kisheria katika kipindi hicho,” alisema Jaji Malata.

Amesisitiza kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa hatakiwi kutenda kosa lolote la jinai, na endapo atakiuka masharti hayo atalazimika kutumikia adhabu hiyo gerezani.

Kesi hiyo ni miongoni mwa tatu za mwanzo kutolewa hukumu na Mahakama Kuu, Kanda ya Songwe tangu kuanza rasmi shughuli zake za kimahakama Machi 30, 2026.

Awali, wakili wa utetezi, Moses Mwampashi aliiomba mahakama imuonee huruma mshtakiwa, akieleza kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na halikupangwa bali lilitokana na mazingira ya tukio.

Aidha, amesema mshtakiwa ana watoto wanne aliowazaa na marehemu, ambao wanamtegemea baada ya kupoteza mzazi wao wa kiume, hivyo kuiomba mahakama izingatie masilahi ya watoto hao katika kutoa hukumu.