NIDHAMU kwanza. Ni kauli ya Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga akielezea mkakati wake wa kuisuka timu hiyo kuhakikisha inabaki salama Ligi Kuu Bara.
Mayanga ametambulishwa usiku wa Aprili 21, 2026 kuchukua nafasi ya Mecky Maxime aliyeachana na timu hiyo ikiwa ni muda mfupi tangu kikosi hicho kifungwe mabao 6-0 dhidi ya Yanga, mechi ikipigwa Aprili 16, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza leo Aprili 22, 2026 wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Isyesye jijini Mbeya, Mayanga amesema anaendeleza walipoishia wengine japokuwa hesabu ni kubaki Ligi Kuu.
Amesema kazi yake kikosini humo ni kushirikiana na wenzake kwenye benchi, wachezaji na uongozi, huku akikiri kuwa kazi si nyepesi lakini kila kitu kinawezekana akiomba sapoti ya mashabiki.
“Kwanza nidhamu ya kujituma kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi, najua tunayo kazi kubwa ya kufanya na tayari timu ina pointi, kwa maana ina kianzio, hivyo mimi nitaendeleza walipoishia wenzangu,” amesema Mayanga.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu hiyo ikiwa Ligi ya Championship kabla ya kutimkia Mashujaa FC msimu uliopita ulipokuwa ukielekea ukingoni, ameongeza kuwa, uwepo wa wachezaji wazoefu na chipukizi sambamba na muunganiko wao, wanaweza kubadili upepo mbaya uliopo sasa.
“Nitasimamia imani ya viongozi walioniamini kuhakikisha tunashirikiana vyema, lemgo ni kuona tunabaki salama Ligi Kuu, nitatumia hii wiki moja kufanya niwezavyo ili mechi ijayo Aprili 30 tuweze kufanya vizuri,” amesema Mayanga.
Kwa upande wake kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Hassan Dilunga, amesema wachezaji wana ari na morali kubwa licha ya upepo mbaya wa matokeo uliowapitia akitoa matumaini kwa mashabiki kuwa Mbeya City haishuki daraja.
Amesema kuwa kazi waliyonayo wachezaji ni kupambania timu kupata matokeo mazuri akikiri kuwa wanafahamu mashabiki hawajafurahi kwani walichotarajia hawajakipata.
“Kusema timu inashuka si sahihi, tunayo ari na morali na kocha huyu tunaamini atatusaidia, jukumu letu ni kupigania timu mechi zilizobaki tuweze kufanya vizuri,” amesema nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga.
Naye kipa wa timu hiyo, Hashim Mussa, amesema mechi zilizobaki ni vita ya fainali kusaka pointi tatu ili kufikia malengo yao ya kuinusuru timu kutoshuka daraja.
“Kikubwa ni kufuata maelekezo ya kocha, kiu yetu ni kupambana kwa sababu kila mechi zilizobaki ni kama fainali ya pointi tatu, lengo ni kubaki salama Ligi Kuu, nafasi tuliyopo si nzuri sana,” amesema kipa huyo aliyewahi kucheza Mbao FC.
Msimu huu wa 2025-2026 ambao Mbeya City imerejea Ligi Kuu Bara, imekusanya pointi 17 baada ya kucheza mechi 19 ikishika nafasi ya 14 ikiwa kwenye hatari ya kurejea Ligi ya Championship, ikibakiwa na mechi 11.