‘Wagonjwa wa himofilia msiwapeleke kwa waganga’

Shinyanga. Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timothy Sosoma amewatahadharisha wananchi kuwapeleka wagonjwa wa himofilia kwa waganga wa jadi badala ya hospitali, akisisitiza kuwa kuchelewa kupata tiba kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwamo kupoteza maisha.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 22, 2026 amesema: “Hadi sasa Mkoa wa Shinyanga una wagonjwa wanne waliobainika kuwa na himofilia. Ni muhimu kwa wataalamu wa afya waliopatiwa mafunzo kuhakikisha wanatoa huduma sahihi kwa wagonjwa hawa.”

Amesema ugonjwa huo ni wa kurithi na hauhusiani na imani za kishirikina, akitoa wito kwa jamii kuachana na mitazamo potofu, badala yake kuwapeleka wagonjwa hospitalini kwa matibabu stahiki.

Chama cha Himofilia Tanzania kimesema ugonjwa huo husababisha damu kushindwa kuganda, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa anapopata jeraha, ikiwamo kusababisha ulemavu au kifo iwapo hatapata matibabu kwa wakati.

Mratibu wa Mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za magonjwa ya damu na Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania, Dk Abdallah Makalla (Mwenye miwani) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki ya Himophilia na seli mundu mkoani Shinyanga.

Akizungumza katika uzinduzi wa kliniki ya kuwahudumia wagonjwa wa himofilia katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Katibu wa chama hicho, Abdallah Makala amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni hatua muhimu ya kusogeza tiba karibu na wananchi wenye uhitaji.

Makala amesema takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10,000 ana tatizo la himofilia.

Amesema kwa kuzingatia idadi ya watu nchini, Tanzania inaweza kuwa na wagonjwa kati ya 6,700 hadi 13,000.

Hata hivyo, amesema hadi sasa wagonjwa waliobainika ni 631 pekee na wanaendelea na matibabu.

“Mgonjwa wa himofilia huishi na ugonjwa huo maisha yake yote, lakini tatizo la kutokwa damu mfululizo linaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi. Gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja kwa mwaka hufikia Sh milioni 243,” amesema Makala.

Ameongeza kuwa, katika mwaka uliopita, chama hicho kilipokea dawa zenye thamani ya Sh120 bilioni kutoka kwa wafadhili, hususan World Federation of Hemophilia, hatua iliyosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa nchini.

Baadhi ya wananchi wameeleza changamoto walizokutana nazo kabla ya kupata uelewa wa ugonjwa huo.

Neema Nicolaus, mkazi wa Shinyanga mwenye mtoto anayeugua himofilia, amesema awali alimpeleka mtoto wake kwa waganga wa tiba za asili akidhani amelogwa, hali iliyosababisha mtoto kupata ulemavu.

“Baada ya kupata elimu, nilimpeleka hospitali na kugundulika kuwa ana himofilia. Alipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Kanda Bugando. Nashukuru sasa huduma imeanza kupatikana hapa Shinyanga,” amesema.

Rejina Shirima ameomba Serikali kuongeza uwekezaji katika tiba ya ugonjwa huo, akieleza kuwa, dawa zake ni ghali na kuna hofu ya huduma kukosekana iwapo wafadhili watajiondoa.

Kwa upande wake, mganga wa tiba asili, Mabula Joseph amesema baada ya kupewa elimu kuhusu himofilia, wataacha kuwahudumia wagonjwa wa aina hiyo badala yake watawashauri kwenda hospitali kupata matibabu sahihi.

Makala amesema pamoja na uzinduzi wa kliniki hiyo, wamewapatia mafunzo wataalamu wa afya kuhusu utoaji huduma kwa wagonjwa wa himofilia, sambamba na kutoa vifaa mbalimbali ikiwamo vitendanishi vya maabara, vifaa vya mazoezi ya viungo, friji za kuhifadhia dawa na kompyuta za kutunzia kumbukumbu za wagonjwa.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuwezesha mazingira mazuri ya ushirikiano na wafadhili, akiwamo Novo Nordisk, pamoja na Muhimbili National Hospital na wadau wengine, katika kuboresha huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya damu nchini.