Wasomi wafichua sababu za nafuu bei ya mafuta Tanzania

Ingawa kupanda kwa bei ya mafuta ni janga linaloyakabili mataifa yote duniani, angalau Tanzania inaonekana kuwa na unafuu wa bei ya nishati hiyo, ukilinganisha na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuanzia Aprili mwaka huu, bei ya lita moja ya petroli kwa Dar es Salaam ni Sh3,820 kwa lita, dizeli Sh3,650 na mafuta ya taa ni Sh3,400 kwa lita.

Bei hiyo ni nafuu zaidi ukilinganisha na Rwanda ambako bei ya lita moja ya petroli kwa Aprili imefika RWF 2,303 (sawa na Sh4,600), dizeli RWF 2,200 (Sh4,400) na mafuta ya taa RWF 2,050 (Sh 4,100).

Kwa upande wa Kenya, taarifa ya Aprili 15 hadi Mei 14, 2026, inaonyesha bei ya lita moja ya petroli ni KSh206.97 (sawa na Sh3,830), dizeli ni KSh193.13 (Sh 3,573) na mafuta ya taa KSh163.71 (Sh 3,029).

Unafuu huo wa bei kwa Tanzania ukilinganisha na baadhi ya nchi Afrika Mashariki, unahusishwa na masuala ya sera, miundombinu na mifumo ya usimamizi wa nishati, kama inavyofafanuliwa na wachambuzi na wanazuoni wa uchumi.

Kupanda kwa bei ya mafuta duniani, kunachochewa na vita inayoendelea Mashariki ya Kati, ikihudisha mataifa ya Marekani, Israel dhidi ya Iran. Vita hiyo imeathiri mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inatoka ukanda huo.

Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania, tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa na Serikali kupunguza matumizi ya nishati hiyo. Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza kupunguza msafara wake uliokuwa unahusisha maofisa waliokuwa wanamfuata kwa magari ya ofisi zao. Agizo hilo pia limeelekezwa kutumika kwenye taasisi zingine kwa maofisa kupunguza matumizi ya magari.

Hilo limefanyika, wakati Serikali ikiendelea na hatua za majadiliano na tathmini kuja na kauli moja itakayoleta unafuu wa bei ya nishati hiyo nchini. Lakini, Serikali imeshatoa hakikisho la kuwepo kwa akiba ya kutosha ya mafuta, itakayofaa kwa zaidi ya miezi mitatu.

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa uchumi, Dk Baraka Mfinanga, ameeleza sababu ni nafasi ya kijiografia ya Tanzania, inayoifanya kuwa lango kuu la mafuta kwa nchi nyingi za Afrika.

“Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la mafuta kwa nchi nyingi za Afrika. Hii inapunguza gharama za usafirishaji kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na nchi zisizo na bandari kama Rwanda,” amesema.

Kwa mujibu wake, gharama ndogo za uingizaji mafuta hupunguza mzigo unaoishia kwa mlaji wa mwisho. Ameongeza kuwa mbali na uwepo wa bandari, Tanzania pia imewekeza katika miundombinu ya uhifadhi wa mafuta, hali inayopunguza utegemezi wa uagizaji wa haraka wa mafuta wakati bei za dunia zinapopanda ghafla.

“Unapokuwa na akiba ya kutosha, unaweza kununua mafuta kwa bei ya chini kabla ya mabadiliko makubwa ya soko, na hivyo kulinda watumiaji wa ndani,” amesema.

Aidha, mwanazuoni huyo, amesema anaiona nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa mafuta kwa nchi jirani kama Uganda na Rwanda inaongeza ufanisi wa soko.

Wingi wa shehena zinazopita nchini huongeza uchumi wa kiwango, hali inayosaidia kupunguza gharama kwa kila lita ya mafuta.

“Kadri unavyopokea na kusambaza mafuta kwa kiwango kikubwa, ndivyo gharama za uendeshaji zinavyogawanyika na kushuka,” amesema.

Kwa upande wake, Mtafiti wa Sera za Uchumi, Neema Kalinga, ameeleza mfumo wa kodi nchini Tanzania una mchango mkubwa katika kudhibiti bei.

“Ingawa kuna tozo mbalimbali, Serikali imekuwa ikifanya marekebisho ya mara kwa mara ili kuhakikisha bei hazipandi kupita kiasi. Hii ni tofauti na baadhi ya nchi ambazo kodi zake ni kubwa na hazibadiliki kirahisi,” amefafanua.

Mchambuzi wa uchumi, Profesa Benedict Mongula, amesisitiza umuhimu wa uthabiti wa sarafu. Ameeleza Shilingi ya Tanzania imekuwa na mabadiliko ya taratibu ukilinganisha na sarafu nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki.

“Unapokuwa na sarafu inayoyumba sana, gharama za uagizaji mafuta hupanda haraka. Tanzania imeweza kwa kiasi fulani kudhibiti hilo,” amesema.

Naye, mchambuzi wa masuala ya biashara na usafirishaji, Hassan Mwakyusa, amehusisha hali hiyo na suala la ushindani wa soko.

Amesema Tanzania ina watoa huduma wengi wa mafuta, jambo linalosaidia kuweka ushindani unaopunguza bei.

“Kadiri washindani wanavyoongezeka, ndivyo inavyokuwa vigumu kwa bei kupanda kiholela. Hii imekuwa tofauti kidogo na baadhi ya nchi jirani ambazo soko lina watu wachache,” amesema.