Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kueleza kwamba imebaini ongezeko la uingiaji na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, shehena nyingine ya dawa hizo imekamatwa ikiwa inaingizwa nchini kutokea Mombasa nchini Kenya.
Dawa hizo zilizokuwa zimefungashwa kwenye vifurushi 1,062 na kuwekwa kwenye viroba 18 zilikamatwa kwenye boti ya kisasa katika ufukwe wa Magambani eneo la Kaole Ufundi Bagamoyo.
Sambamba na dawa hizo wamekamatwa pia watuhumiwa wanne ambao wote ni raia wa Tanzania, wawili wakiwa wakazi wa Tanga na wengine wawili wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Hili linakuja baada ya DCEA kubaini kukua kwa mtandao wa biashara ya mirungi na kusababisha uingizaji wa dawa hizo kuongezeka nchini ambapo kwa Machi pekee kilogramu 1267.12 zilikamatwa.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kukamatwa kwa boti hiyo usiku wa kuamkia Aprili 14, 2026 matokeo ya operesheni iliyofanyika kuubaini mtandao wa biashara ya mirungi nchini ambayo inaonekana kushika kasi siku za karibuni.
Amesema baada ya kazi kubwa kufanyika katika kutokomeza dawa za kulevya za viwandani na bangi, sasa hivi matumizi yameongezeka kwa kasi kwenye mirungi hivyo mbinu mbalimbali zinafanyika kuingiza dawa hizo nchini.
Lyimo amesema operesheni hiyo ilifanyika baada ya kupatikana kwa taarifa kuhusu uwepo wa mtandao unaojihusisha na uingizaji wa dawa hizo kupitia njia za majini.
Baadhi ya vifurushi vya dawa za kulevya aina ya mirungi vikiwa vimekamatwa kwenye ufukwe wa Magambani Kaole Ufundi wilayani Bagamoyo.
Ameeleza kuwa kikosi maalumu kilifuatilia kwa karibu mienendo ya boti hiyo hadi ilipofika katika eneo la Kaole, ambapo ilizingirwa na kukamatwa.
“Hii boti kwa muda mrefu imekuwa ikisafirisha mirungi kutoka Kenya kuja Tanzania, tumekuwa tuliifiatikia na hatunaye tumefanikiwa kuikamata ikiwa na mzigo wake wote. Hii ni hatua kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. Tunaendelea kuwafuatilia wahusika wote waliokuwa nyuma ya biashara hii haramu,” amesema.
Kamishna Jenerali huyo amebainisha kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini mtandao ulioratibu usafirishaji huo, ikiwa ni pamoja na kuwabaini wafadhili, wasambazaji na wapokeaji wa mzigo huo nchini.
“Kwa namna yoyote ile hatutavumilia vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama na afya ya wananchi na kwamba yeyote atakayebainika kuhusika na biashara ya dawa za kulevya atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali hadhi yake.
“Niwasihi wananchi kuendelea kuwa macho na kuripoti matukio yoyote yanayohusiana na dawa za kulevya, ikisisitiza kuwa mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu yanahitaji nguvu ya pamoja.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kaole Ufundi Hamad Urali amesema tukio hilo limewastua wengi, akieleza kuwa eneo hilo limekuwa likionekana tulivu kwa muda mrefu.
“Hatukuwahi kufikiria kama kuna mambo kama haya yanaweza kufanyika hapa. Inaonyesha jinsi mitandao hii ilivyojipanga kwa siri,” amesema Urali.
Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa masuala ya kijamii, Dk Amina Khamis amesema kukamatwa kwa mzigo huo ni ishara kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya bado ni kubwa na inahitaji ushirikiano wa wadau wote.
Baadhi ya vifurushi vya dawa za kulevya aina ya mirungi vikiwa vimekamatwa kwenye ufukwe wa Magambani Kaole Ufundi wilayani Bagamoyo.
Amesema matumizi ya mirungi, hasa kwa vijana yamekuwa yakichangia matatizo ya kiafya na kijamii, ikiwa ni pamoja na utegemezi wa dawa, kupungua kwa uzalishaji na kuongezeka kwa uhalifu mdogo mdogo.
“Ni muhimu jamii ikaendelea kutoa taarifa pale wanapohisi kuna harakati za aina hii. Vyombo vya dola haviwezi kufanikiwa peke yake bila ushirikiano wa wananchi,” amesema Dk Amina.
