Mafuriko yakata mawasiliano Korogwe | Mwananchi

Korogwe. Mawasiliano katika barabara kuu ya Tanga–Arusha yamekatika kutokana na mvua zilizonyesha kwa saa tisa mfululizo na kusababisha Mto Mbeza kufurika, hali iliyosababisha shughuli za kiuchumi kusimama.

Mafuriko hayo pia yameingia katika Soko la Manundu na kusababisha uharibifu wa bidhaa, huku tathmini kamili ya hasara hiyo ikiwa bado haijafanyika hadi sasa.

Wakizungumza katika eneo la tukio, baadhi ya wananchi, akiwemo Samweli Mweta, wamesema shughuli za kiuchumi zimesimama kufuatia mto huo kufurika, na kuiomba Serikali kushughulikia adha hiyo ambayo sasa imekuwa kero ya kudumu.

“Kwa adha hii ambayo imetokea hapa, imetusababisha tushindwe kuendelea na shughuli zetu za kiuchumi. Hii ni mara ya pili sasa adha hii inatokea na kusababisha athari kwa wananchi,” amesema mmoja wa wananchi hao.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Semkiwa, Agnes Charange amesema wameshindwa kupita katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kuhudhuria masomo, akieleza kuwa hali hiyo inaathiri maendeleo yao kitaaluma kwa kuwa si mara ya kwanza kutokea.

“Mimi niliamka asubuhi sana kwenda shule, lakini leo nimefika hapa nimekuta hapapitiki kabisa, kwa hiyo jambo hili naomba lipewe kipaumbele ili lisitokee tena,” amesema mwanafunzi huyo.

Mto Mbeza ukiwa umefurika kutokana na mvua zilizonyesha kwa saa tisa Korogwe.

Kwa upande wa wasafirishaji, akiwemo Ibrahim Hussein anayefanya safari zake kati ya Chalinze na Arusha, amesema hawajui hatma yao kutokana na mawasiliano kukatika huku mvua zikiendelea kunyesha.

“Hatujui tunaondoka hapa saa ngapi, kwa maana mvua bado zinaendelea kunyesha. Abiria wanalalamika, lakini tufanyeje wakati mvua bado zinaendelea kunyesha,” amesema Hussein.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Korogwe Mji, Ally Mkwavingwa, amesema tayari jitihada zimeanza kuchukuliwa baada ya tatizo hilo kujitokeza mara mbili mfululizo na kuathiri wasafiri, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Tatizo hili linajitokeza kwa mara ya pili sasa kutokana na mto kujaa mchanga na kupoteza mkondo wake, hali inayosababisha maji kuingia kwenye makazi ya watu na kuleta madhara makubwa,” amesema Mkwavingwa.

Daraja lililoharibika kutokana na mafuriko.

Kufurika kwa mto huo kumesababisha athari kubwa kwa wafanyabiashara wa Soko la Manundu pamoja na watumiaji wa barabara kuu ya Tanga–Arusha, huku wadau wakisisitiza kuwa upatikanaji wa ufumbuzi wa kudumu utasaidia kufanya matukio ya aina hii kuwa historia.