Mbozi kuimarisha matumizi ya vyoo bora, usafi wa mazingira

Mbozi. Wadau wa mazingira wilayani Mbozi, mkoani Songwe, wametakiwa kuhamasisha jamii kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira ili kudhibiti athari za uchafuzi, zikiwamo magonjwa ya mlipuko na vifo vinavyotokana na magonjwa hayo.

Wito huo umetolewa leo Aprili 15, 2026 katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mbozi, kikihusisha viongozi wa mila na dini, wazee maarufu, wakuu wa idara na vitengo, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, pamoja na Shirika la Sawa (Sanitation and Water Action). Kikao hicho kiliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega.

Akifungua kikao hicho, Mbega amesema lengo ni kuwashirikisha wadau ili kuufikisha kwa urahisi ujumbe wa ujenzi wa vyoo bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa elimu itolewe kwanza kabla ya kuchukua hatua za kisheria kwa wanaokiuka. Amekemea tabia ya baadhi ya kaya kukosa vyoo na kujisaidia vichakani, akisema hali hiyo ni hatari kwa afya ya jamii.

Kwa upande wake, msimamizi wa miradi kutoka Sawa, Wilhelmina Malima, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wadau uwezo wa kuhamasisha jamii kuhusu usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo bora. Amebainisha kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa wananchi, hivyo elimu inaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ili kubadilisha mitazamo.

Mwenyekiti wa mazingira upande wa machifu, Hazole Msyete, amesema ushirikiano hafifu kati ya watendaji wa serikali na viongozi wa mila unakwamisha juhudi za utunzaji wa mazingira. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ukiimarishwa, utekelezaji wa mikakati utafanikiwa.

Wadau hao wamekubaliana kutumia mikutano ya hadhara na ya vijiji kutoa elimu kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira.