Dk Gwajima asimulia anavyozikabili lugha chafu mitandaoni-3

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema maneno makali na lugha chafu anazokutana nazo katika mitandao ya kijamii, anazichukulia kuwa kiashiria cha ukubwa wa changamoto zinazowakabili wananchi.

Kwa kulitambua hilo, amesema wakati mwingine hulazimika kuwasikiliza hata wale wanaotumia lugha kali au isiyo na staha dhidi yake.

Amesema kufanya hivyo, kunamsaidia kuwapa nafasi ya kumwaga yaliyomo mioyoni mwao na kufahamu kwa undani kiini cha changamoto wanazopitia.

Dk Gwajima amesema hayo katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Amesema licha ya jumbe nyingi za pongezi anazopokea kutoka kwa wananchi kupitia mitandao yake ya kijamii, pia wengine hutoa maoni makali, kejeli au hata mashambulizi binafsi dhidi ya viongozi.

Amesema katika hali hiyo, amejifunza kutofautisha kati ya lugha inayotumika na ujumbe uliomo ndani yake, akieleza kuwa mara nyingi hata maneno makali hubeba ujumbe muhimu unaopaswa kufanyiwa kazi.

“Ukijikita kwenye namna mtu alivyosema unaweza kupoteza hoja. Lakini ukisikiliza kwa makini, unaweza kupata kiini cha tatizo,” amesema waziri huyo.

Dk Gwajima ameongeza kuwa, baadhi ya watu wanaotoa maoni hayo wanaweza kuwa wanapitia changamoto zao binafsi, hivyo kiongozi anapaswa kuwa na huruma na uvumilivu badala ya kujibu kwa hasira.

“Huwezi kujua mtu yuko katika hali gani. Anaweza kuwa na msongo wa mawazo au amechoka kutafuta msaada bila mafanikio, hivyo anaamua kuwasilisha kwa namna hiyo,” amefafanua.

Amesema katika baadhi ya matukio ambayo mijadala inakuwa mikali, huchagua kuwasiliana na wahusika kwa njia ya faragha ili kuelewa undani wa tatizo na kulipatia ufumbuzi unaofaa.

“Ukimfuata mtu kwa utulivu, mara nyingi anakwambia ukweli wote na hapo ndipo unapoweza kumsaidia vizuri zaidi,” amesema Dk Gwajima.

Amesema katika mazingira ya sasa, mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa lisiloepukika kwa kiongozi anayehitaji kusikia sauti ya wananchi bila vikwazo vya taratibu ndefu za kiutawala.

“Leo hii mtu anakutumia ujumbe au video, unaliona jambo palepale lilipotokea. Hapo huwezi kusema ngoja kesho, kwa sababu tayari umeshajua,” amesema.

Amefafanua kuwa, mara nyingi taarifa anazopokea kupitia mitandao hiyo zinahusu hali halisi inayogusa maisha ya watu, ikiwamo migogoro ya kifamilia, ukatili wa kijinsia, malezi ya watoto na masuala ya ustawi wa jamii kwa jumla.

Kwa mujibu wake, kasi ya upatikanaji wa taarifa hizo imepunguza utegemezi wa mlolongo wa kawaida wa kiutawala ambao mara nyingi huchukua muda mrefu kabla ya hatua kuchukuliwa.

Akitoa mfano wa tukio lililoripotiwa mkoani Arusha la kijana aliyedaiwa kumpiga mwanafunzi, amesema alipokea video ya tukio hilo kupitia mitandao ya kijamii na kuchukua hatua haraka kwa kuwasiliana na mamlaka husika, jambo lililosaidia kuharakisha uchunguzi na hatua stahiki kuchukuliwa.

“Kwa mfumo wa kawaida, taarifa ingepitia ngazi nyingi kabla ya kufika kwa wahusika. Lakini kupitia mitandao, unawafikia wote kwa wakati mmoja na hatua zinaanza kuchukuliwa mara moja,” amesema.

Hivyo, waziri huyo anasisitiza mitandao ya kijamii ni chombo muhimu cha kuharakisha mawasiliano na kuongeza uwajibikaji kwa viongozi.

“Nasema hivyo kwa sababu wananchi sasa wanapata nafasi ya kueleza matatizo yao moja kwa moja,” amesema.

Na pia, Waziri Gwajima amesema kupitia jukwaa hilo, anaweza kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja tofauti na mikutano ya ana kwa ana ambayo ina mipaka ya idadi ya watu na muda.

“Posti moja inaweza kufikiwa na maelfu ya watu, na wengi wao wakatoa maoni au taarifa zinazoweza kusaidia kutatua tatizo kwa haraka zaidi,” amesema.

Hata hivyo, amesema mitandao ya kijamii si mbadala wa mifumo rasmi ya Serikali, bali ni nyongeza inayosaidia kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Muda gani anatumia mitandao

Akizungumzia muda anaoutumia kwenye mitandao hiyo, amesema hana muda maalumu kwa kuwa anapatikana muda wote akifuatilia taarifa na kujibu ujumbe unaomfikia.

“Taarifa zikiingia naziona na kulingana na uzito wa jambo nachukua hatua. Huwezi kusema utashughulikia jambo kesho wakati tayari umeliona leo,” amesema.

Amesema baadhi ya wananchi humfuata moja kwa moja kupitia ujumbe binafsi (DM), jambo linalomwezesha pia kupata maelezo ya kina kuhusu changamoto zao na kuchukua hatua zinazofaa kwa haraka zaidi.

Wito kwa viongozi wenzake

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wenzake kutoikimbia mitandao ya kijamii kutokana na hofu ya kukosolewa au kushambuliwa, akisisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya uongozi wa kisasa.

“Watu watasema mengi, lakini muhimu ni kuangalia hoja. Ukisaidia kutatua tatizo lao, wataacha kuangalia madhaifu yako na wataona nguvu yako,” amesema.

Amesema katika wizara yake ameanza kuchukua hatua za kuhakikisha maofisa ustawi wa jamii wanatumia teknolojia kwa kuwapatia vifaa vya mawasiliano vilivyounganishwa kidigitali katika mikoa yote 26, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi katika kushughulikia changamoto za wananchi.

Ameongeza kuwa mpango huo unatarajiwa kushushwa hadi ngazi ya wilaya ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa haraka zaidi.

Mbali na masuala ya kazi, Dk Gwajima pia amezungumzia maisha yake binafsi, hususan uhusiano wake na mume wake ambao umekuwa ukionekana mara kwa mara hadharani.

Amesema hatua ya kumhusisha mume wake katika shughuli zake ni sehemu ya kuonesha kwa vitendo yale ambayo wizara yake inahubiri kuhusu umuhimu wa familia na malezi bora.

“Sera tunazozisimamia zinahusu familia, hivyo ni muhimu na sisi kuonesha mfano kwa vitendo,” amesema.

Amesema uwepo wa mume wake katika maisha yake unampa utulivu wa akili na kumsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Amesema wanapochapisha picha au video zao wakiwa pamoja, baadhi ya watu hutoa maoni mbalimbali, lakini wao wanachukulia hali hiyo kama ishara kuwa ujumbe wanaotaka kuufikisha, unawafikia wananchi.

Akitoa ushauri kwa vijana, Waziri Gwajima amesema ni muhimu kwao kujenga urafiki, uwazi na uaminifu kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa ndoa.

“Uhusiano bora huanza na urafiki. Lazima mjengane katika uaminifu na uwazi,” amesema.

Ameonya kuwa ukosefu wa maadili na uwazi katika familia unaweza kuathiri malezi ya watoto na hatimaye jamii kwa jumla.

Amesisitiza kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha anachangia katika kujenga familia imara na jamii yenye maadili.

Aidha, amewataka vijana kuishi maisha yao kwa uangalifu wakitambua kuwa matendo yao ya sasa yanaweza kuwa na athari kwa vizazi vijavyo.

“Jiulizeni, maisha mnayoishi leo, mnatamani watoto wenu waje kuyaishi? Kama sivyo, basi badilikeni,” amesema Dk Gwajima.