Unguja. Jeshi la Polisi Zanzibar linaendelea kumshikilia na kumhoji Joe McCann, aliyekuwa mpenzi wa mhamasishaji wa mitandao ya kijamii Ashly Robinson maarufu Ashlee Jenae kutoka Marekani.
Wapenzi hao walifika Zanzibar Aprili 4, 2026 kwa ajili ya kutalii na walifikia katika hoteli ya kitalii ya Zuri, Mkoa wa Kaskazini Unguja lakini walitofautiana hatua iliyosababisha Ashlee kujinyonga.
Kwa mujibu wa polisi, kabla ya kujinyonga uongozi wa hoteli ulichukua hatua ya kuwatenganisha vyumba na kila mmoja akiwa na chumba chake ambapo Aprili 9 ndio Ashlee alibainika akiwa amejifunga na kitambaa cha nguo yake juu ya kabati akitaka kujiua.
Jana Jumanne, Aprili 14, 2026, mwili wa binti huyo ulikuwa unamaliziwa kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kwa kushirikiana na ubalozi wa Marekani polisi na wataalamu wa afya.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera amesema pasi ya kusafiria ya kijana huyo wanaishikilia wakiendelea kumhoji.
Alipoulizwa na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 15, 2026 hatua zilizofikiwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini, Benedict Mapujira amesema bado upelelezi unaendelea na kumhoji mchumba wake hivyo wakimaliza watatoa ripoti.
“Ukiniuliza kilichobainika huo ndio upelelezi wenyewe, sasa unataka tuanze kueleza masuala ya upelelezi kwenye vyombo vya habari.
Bado tunaendelea na upelelezi na upelelezi kama huo hauwezi kukamilika kwa siku moja, kwa hiyo tusubiri itatolewa ripoti kamili baada ya kukamilisha,” amesema Kamanda bila kutaka kuingia ndani zaidi kwa madai ni kuingilia upelelezi.
Mmarekani huyo anadaiwa kujinyonga Aprili 9, 2026 akiwa katika hoteli za kitalii kisiwani hapa Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya kutofautiana na mchumba wake kisha alikimbizwa hospitali na akafariki dunia April 10, 2026.
Hata hivyo, familia ya Ashlee imekuwa na kauli tofauti kuhusu maelezo hayo ikimshutumu mchumba wake kwamba ndiye anahusika na kifo hicho.
