Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa andiko la mradi wa ‘Sifa’ utakaokarabati shule zote chakavu za awali, sekondari, msingi na kongwe.
Ameeleza hayo wakati wa kuchangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahitimishwa leo Jumatano Aprili 15, 2026, bungeni jijini Dodoma.
Mchango wa Profesa Shemdoe ulikwenda sambamba kujibu hoja za wabunge mbalimbali waliokuwa wakichangia bajeti hiyo ya Sh12.5 trilioni kubainisha maboma na miundombinu ya shule kutoridhisha.
Profesa Shemdoe amesema tathimini iliyofanyika imebaini ukarabati unaohitajika kwa shule ya msingi katika vyumba vya madarasa 42,716 na nyumba za walimu 31,813.
Wakati upande wa shule za sekondari vyumba vya madarasa 6,889 na nyumba za walimu 3,518, maktaba 91 na mabweni 309.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya elimu kwa awamu, kati ya mwaka 2021/22 hadi 26 Serikali imetumia Sh 237.9 bilioni.
“Namshukuru Profesa Kitila (Mkumbo- Waziri wa Mipango) na timu yake kwa kulikubali andiko hili ili litafutiwe fedha za kuanza utekelezaji kwa nchi nzima,” amesema Profesa Shemdoe.
Kuhusu watu wenye ulemavu kukosa mikopo, Profesa Shemdoe amesema wamelifanyia kazi suala hilo na kueleza kuwa kwa sasa mtu mmoja mmoja mwenye changamoto hiyo, anaweza kupata mkopo ili kutoa nafasi ya kunufaika.
“Suala hili limeendelea kufanyiwa kazi na lina suluhisho lake mheshimiwa Spika (Mussa Zungu),” amesema.
Mbali na hilo, Profesa Shemdoe amesema Serikali imefanya tathimini wa barabara zinazomilikiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na kubaini Sh99.636 bilioni zinazohitaji kurekebisha miundombinu hiyo iliyoharibiwa na mvua.
Profesa Shemdoe amesema wamekaa na wizara zinazohusika ikiwemo ya Mipango ili kuhakikisha fedha hizo zinapatikana kwa ajili ya kurekebisha barabara hizo.
Awali, akichangia mjadala huo na kujibu hoja za wabunge, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema bajeti ijayo ya wizara hiyo, wametoa kipaumbele katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa ruzuku na pembejeo.
Pia, Chongolo amesema wametoa kipaumbele cha kutenga fedha za kulipa madeni ya fedha za ruzuku kwa mawakala na wasambazaji wa mbolea kuongeza wigo wa upatikanaji wa mbolea ili kuwapunguza usumbufu na gharama.
“Tutahakikisha tunawekeza kwenye upatikanaji wa mbegu bora ili kupunguza mbegu feki. Kuhusu ununuzi wa nafaka za mahindi, mwaka huu tumenunua mahindi ya Sh95.3 bilioni na sasa tumeshalipa Sh93.1 bilioni,”
“Dhamira ya wizara ni kuhakikisha inaendeleza kilimo, ili kuwanufanisha wakulima kujikwamua na umasikini,” ameeleza Chongolo.