Wanazuoni waja na njia kufanya tafiti ziwe injini ya maendeleo

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikielekea kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayoweka msisitizo katika tafiti kufikia maendeleo endelevu, wanazuoni waja na njia mbadala za kuhakikisha tafiti zinageuka kuwa injini ya maendeleo badala ya kubaki kwenye makabrasha.

Hatua hiyo ya wasomi inakuja ikiwa kwa muda mrefu, kumekuwepo na ongezeko la tafiti katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, lakini wachambuzi wakieleza kuwa nyingi zimekuwa hazina matokeo ya moja kwa moja kwa jamii, hali inayochangia kuendelea kwa changamoto za kiuchumi na kijamii.

Mjadala huo umechukua sura mpya kufuatia kongamano la kwanza la kimataifa lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Aprili 15, 2026 chini ya mradi wa Creating a Joint Infrastructure for Dialogue, Research and Advocacy (CIDRA), unaolenga kuunganisha nguvu za watafiti kutoka Afrika na Ulaya.

Aidha, mjadala huo uliowakutanisha wanazuoni kutoka vyuo vikuu 13 Afrika na Ulaya, unaibua matumaini kwa Tanzania kwani, Serikali kupitia Wizara ya Elimu imekuwa ikisisitiza mabadiliko ya dhati katika sekta ya tafiti, ikitaka tafiti zielekezwe kwenye maeneo yenye tija na zinazoweza kusaidia utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa 2050 inayoweka maarifa na ubunifu kama nguzo muhimu ya uchumi.

Wakizungumza katika kongamano hilo lililolenga kujadili mchango wa sera na sheria katika maendeleo ya pamoja baina ya Afrika na Ulaya, wadau wameeleza namna CIDRA inavyokwenda kuendesha tafiti na mijadala ya kimataifa itakayofanya tafiti za kitaaluma kutoa matokeo badala ya nadharia za wasomi zisizokuwa na mchango katika maisha ya watu.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mhadhiri mwanadamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bernadetha Kilian, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo hicho, amesema dunia ya sasa inayoendeshwa na kasi ya teknolojia inahitaji tafiti zenye uwezo wa kutoa majibu ya haraka na ya vitendo kwa changamoto za jamii.

“Tunahitaji tafiti zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja katika teknolojia, mazingira na mifumo ya kidijitali ili ziweze kubadili jamii zetu,” amesema.

Kauli hiyo inaakisi pengo lililopo, ambapo tafiti nyingi zimekuwa za kinadharia zaidi kuliko za kimatokeo, huku zikikosa uhusiano wa moja kwa moja na watunga sera na watekelezaji.

Akifafanua namna mradi wa CIDRA unavyolenga kujibu changamoto hiyo, Dk Steven Kirama, mhadhiri mwandamizi wa Shule Kuu ya Uchumi (SOEC) UDSM na msimamizi wa mradi huo, amesema mradi huo umejengwa mahsusi kuunganisha tafiti na utekelezaji.

Amesema mradi huo ulioanza mwaka 2023/24 unahusisha vyuo 13 ambapo sita ni kutoka Afrika na saba kutoka Ulaya, akifafanua kuwa unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mfuko wa Erasmus kwa zaidi ya dola za kimarekani milioni moja.

“Tunafanya uchambuzi wa pamoja, kubadilishana maarifa na pia kuwakutanisha watafiti na watunga sera ili kuhakikisha tafiti hizi hazibaki darasani bali zinakuwa sehemu ya maamuzi ya maendeleo,” amesema.

Ameongeza mradi huo pia unajikita katika maeneo muhimu kama ushirikiano wa kiuchumi na nishati jadidifu, huku ukitoa jukwaa la mijadala ya sera kati ya Afrika na Ulaya.

Hii pia inaonesha namna tafiti hizi zitakavyosaidia kusukuma vipaumbele vya Serikali ya Tanzania kwani Rais Samia amewekeza nguvu kubwa katika masuala ya nishati jadidifu hasa nishati safi ya kupikia, ambayo imempaisha kimataifa na kupewa tuzo ya kinara katika eneo hilo kwa Afrika.

Kwa mujibu wa wataalamu, tofauti kubwa ya CIDRA na tafiti za awali ni msisitizo wake katika ushirikiano wa pande mbili, badala ya mfumo wa zamani uliokuwa ukitawaliwa na upande mmoja.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa UDSM, Luka Ramadhani, amesema huu ni mwanzo wa tafiti zenye mwelekeo mpya wa kimataifa zitakazoleta maendeleo kwa jamii.

“Huu ni ushirikiano unaolenga kujenga maarifa ya pamoja, badala ya nchi moja kuongoza nyingine. Hii itasaidia tafiti zetu kuwa na maana zaidi kwa jamii,” amesema.

Akizungumzia muktadha wa Afrika na itakavyonufaika na tafiti hizo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa, Dk Zemelak Ayele, amesema Afrika ina nafasi ya kipekee ya kutumia tafiti kama nyenzo ya kuunganisha maendeleo kutokana na kufanana kwa jamii na changamoto zake.

“Jamii zetu zinafanana kwa changamoto, hivyo tafiti zinaweza kuwa daraja la kutuunganisha na kutuletea suluhisho la pamoja,” amesema.

Ili kutimiza matumaini hayo, wanazuoni hao wamesema kuwa mafanikio ya juhudi hizi yatategemea utekelezaji wake, wakisisitiza kuwa bila hatua madhubuti, tafiti zitaendelea kuwa nyingi lakini zisizo na mchango kwa maendeleo ya wananchi.

Katika muktadha huo, kongamano la CIDRA linaonekana kuwa hatua muhimu ya mwanzo wa mageuzi ya sekta ya tafiti likitoa matumaini kwamba tafiti zinaweza kubadilika kutoka nadharia hadi kuwa nguvu halisi ya maendeleo ya taifa.