Geita. Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Ally Mketo, amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ushirombo kudumisha usafi wa vyoo vipya vilivyojengwa shuleni hapo ili visigeuke chanzo cha magonjwa, sambamba na kujiepusha na vitendo vya ngono katika umri mdogo vinavyoweza kuathiri afya na masomo yao.
Mketo ameyasema hayo leo Aprili 15, 2026 wakati wa hafla ya kukamilika kwa mradi wa vyoo vya wasichana uliotekelezwa na Shirika la The Legal Aid Foundation (LSF) kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wilayani humo, mkoani Geita.
Mradi huo wa jengo lenye matundu manane ya vyoo, uliogharimu Sh25 milioni, ulianza Desemba 16, 2025 na kukamilika Machi 30, 2026, ukilenga kupunguza changamoto ya uhaba wa vyoo iliyokuwa ikiathiri afya, usafi wa mazingira na mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kike.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa LSF, Mkuu wa Fedha na Utawala, Richard Mwakalindile, amesema utekelezaji wa mradi huo umezingatia uhitaji mkubwa uliopo katika Wilaya ya Bukombe, huku akiahidi kuwa miradi kama hiyo itaendelea kutekelezwa katika maeneo mengine nchini.
Mwanzilishi wa taasisi ya Run for Binti na Mkurugenzi wa Smile for Community, Flora Njelekela, amesema shule hiyo ilipewa kipaumbele kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na uhaba wa vyoo, hasa kwa wasichana. Ameongeza kuwa kupitia mbio za hisani za Run for Binti Marathon, wadau waliweza kukusanya fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo pamoja na kuchangia juhudi za utunzaji wa mazingira na kupinga ukatili wa kijinsia.
Katibu Tawala wilaya ya Bukombe,Ally Mketo (mwenye skafu ya Rangi za Bendera ya taifa shingoni) akiongoza uzinduzi wa matundu ya vyoo Shule ya Sekondari Ushirombo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Paskas Mragili.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya Stanbic, Mkoa wa Geita, Hilda Gwimba, amesema taasisi yao ilishiriki kudhamini mradi huo pamoja na upandaji wa miti 800, akisisitiza kuwa kumwezesha mtoto wa kike ni kuwekeza katika maendeleo ya Taifa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Alex Chombe, amesema mradi huo umepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa vyoo, lakini bado wanahitaji mabweni kwa wanafunzi ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.
