Afrika Kusini. Mawakili wa kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, wamewasilisha maombi wakati mchakato wa utoaji hukumu kwa kiongozi huyo ulipoanza katika Mahakama ya Hakimu KuGompo, katika eneo la Eastern Cape, leo Jumatano Aprili 15, 2026.
Hakimu Twanet Olivier amesikiliza hoja za mwisho kutoka kwa upande wa utetezi na upande wa mashtaka kabla ya kuahirisha shauri hilo hadi kesho asubuhi Alhamisi Aprili 16, 2026 kwa ajili ya kutoa hukumu.
Mwendesha mashtaka Joel Cesar ameiambia mahakama kuwa anaomba Malema apewe kifungo cha hadi miaka 15 jela, baada ya kupatikana na hatia Oktoba 2025 kwa makosa matano chini ya Sheria ya Udhibiti wa Silaha za Moto.
Aidha, ameomba adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela, ambapo miaka mitatu itasimamishwa, pamoja na faini kwa makosa yaliyosalia.
Mashtaka hayo yanatokana na tukio la mwaka 2018 katika mkutano wa EFF huko Mdantsane, ambapo Malema alifyatua risasi hewani. Mshtakiwa mwenza, Adriaan Snyman, aliachiliwa huru.
Mahakama ilielezwa hapo awali kuwa Snyman alimkabidhi Malema silaha hiyo wakati wa tukio hilo.
Iwapo Malema atahukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 jela bila chaguo la kulipa faini, atapoteza kiti chake bungeni.
Maelfu ya wafuasi wa EFF walikusanyika nje ya mahakama tangu alfajiri, wengi wao wakiwa wamekesha kwa ajili ya kufanya maombi. Pia, polisi waliweka ulinzi kuzunguka jengo hilo.
Malema aliwasili saa tatu asubuhi akiwa pamoja na timu yake ya wanasheria na viongozi wakuu wa chama.
Wakili Laurance Hodes ameiambia mahakama kuwa mashtaka yote matano yanatokana na tukio moja lililodumu chini ya dakika mbili.
“Kutoa adhabu ya kifungo cha jela kwa tukio moja fupi la aina hii kungekuwa hakukubaliki na kisichoendana na uzito wa tukio,” amesema.
Ameeleza hali binafsi ya Malema, akisema sasa ana miaka 45, alikuwa na miaka 37 wakati wa tukio, hana rekodi ya makosa ya awali na “ameishi maisha yasiyo na lawama.”
Ameongeza kuwa hakujakuwa na matukio mengine kama hayo tangu mwaka 2018.
Hodes ameiambia mahakama kuwa Malema alipokea bunduki hiyo kutoka kwa mtu anayeaminika kuwa na uhusiano na vyombo vya usalama, akieleza kuwa ilikuwa silaha iliyosajiliwa kisheria.
Amesema Snyman alimkabidhi Malema bunduki hiyo, ambaye aliiazima kwa ajili ya tukio hilo, akaishikilia kwa chini ya dakika moja wakati akifyatua risasi na akairejesha mara moja.
