Wizara tatu kutafuta tiba migogoro ardhi

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, amesema tayari wizara hiyo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali wameshaanza vikao vya kutafuta dawa ya migogoro ya ardhi.

Dk Akwilapo, ametoa kauli hiyo akirejea maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyetaka wizara hiyo, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakae kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi nchini.

Dk Mwigulu alitoa maelekezo hayo, akiwa ziarani mkoani Rukwa mwishoni mwa Februari 2026, baada ya kupokea utitiri wa kero zinazohusu migogoro ya ardhi. Alitoa maelekezo hayo baada ya ziara zake zilizoanzia Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kukutana na kero lukuki nyingi zikiwa migogoro ya ardhi.

Dk Akwilapo, ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Aprili 15, 2026 alipochangia mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/27 ya Sh12.5 trilioni, bungeni jijini Dodoma.

Amesema tayari wizara hizo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), zimeshaanza kukutana kwa ngazi ya maofisa kujadili, kuchakata na kutoa ushauri wa namna bora ya kusimamia ardhi bila kusababisha migogoro.

Vikao hivyo, amesema vitafuatiwa na vile vya mawaziri na kisha taarifa itatolewa na kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu.

Dk Akwilapo, amesema wataongeza kasi ya upangaji wa miji na kusimamia kwa ukaribu taratibu za utoaji ardhi kwa kuhakikisha ardhi iliyotwaliwa wananchi wanalipwa fidia.

“Taasisi zote ambazo zitaomba kutwaa ardhi mahali popote, zijiandae ziwe na fedha kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi, ili upimaji na tathimini ikifanyika isichukue muda mrefu wananchi wawe wamelipwa fidia zao,” amesema.

Katika mwaka huu wa fedha, amesema vijiji 253 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na mwaka ujao wa fedha mipango 426 itafanyika.

Amesema upangaji wa mipango hiyo ndiyo suluhisho la migogoro ya wakulima na wafugaji kwa sababu inawahusisha watu wa pande zote kukubaliana wapi pawe pa mifugo na kilimo.

Kuhusu kurahisisha upatikanaji wa hati za ardhi, amesema wanaimarisha mifumo na jumla ya halmashauri 48 zimeshaanza kuwa na mfumo na hiyo itakomesha eneo moja kuwa na hati mbili.

Amesisitiza maeneo mengine yote yaliyochangiwa na wabunge, yatajibiwa katika hotuba ya wizara hiyo itakayotolewa hivi karibuni.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema mafao kwa sekta ya umma, siku za ulipaji zimepungua na kufikia 25 badala ya zaidi ya mwezi.

“Wastaafu walikuwa wanalipwa Sh100,000 kima cha chini, baada ya kuboresha kwa sasa wastaafu wanalipwa kima cha chini Sh250,000 sawa na ongezeko la asilimia 150,” amesema.

Katika mchango wake huo, amegusia Kiwanda cha Mkulazi kinachozalisha sukari, akisema kililalamikiwa ni mufilisi lakini sasa kinazalisha sukari ya viwandani.

Amesema hiyo inakifanya kuwa cha pekee kinachozalisha sukari hiyo na kuondoa nakisi ya asilimia 20 ya sukari ya viwandani inayoagizwa kutoka nje.

“Ajira zaidi ya 11,000 zimepatika ndani ya muda mfupi. Lakini wakulima waliuza tano 37,981 kwa thamani ya Sh2.85 bilioni na mwaka huu wanaenda kuuza tani 53,128 kwa Sh4.06 bilioni.

“Wakulima wale walikuwa na deni kwenye taasisi za fedha la Sh3.24 bilioni, kupitia uwekezaji huu tumefanya mazungumzo na taasisi za fedha na wananchi wanakwenda kutoka kwenye mzigo wa deni na watanufaika na kuwepo kwa kiwanda,” amesema.