BAADA ya kuchezea kichapo cha mabao 0-3 nyumbani kutoka kwa Yanga, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza, amekiri kwamba mechi hiyo imemuachia vidonda vingi.
Pamba Jiji ambayo inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 26, iliikaribisha Yanga Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Dar na kuchezea kipigo hicho.
Lakini kazi iliyoko mbele yao ni mechi dhidi ya TRA United, moja kati ya timu sumbufu na ngumu kufungika, huku ikiweka rekodi ya kuwatoa kapa Yanga na Simba. Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Baraza alisema wachezaji wengi hawakuwa sawa baada ya mechi dhidi ya Yanga, jambo ambalo lilimpa hofu.
Alisema kwa sasa anaiona afadhali kubwa hasa kwa wachezaji ambao walikumbwa na majeraha madogo madogo, hivyo nguvu zinahamia kwa Watoza Kodi.
“Kweli tuna mechi ngumu sana, lakini kwa imani kubwa tutafanya vyema. Napata uhakika zaidi kwa sababu ya hali za wachezaji zilivyo.
“Yanga iliniachia majeraha mengi, nadhani wachezaji walicheza kwa nguvu zote licha ya kupoteza, ila unaona jinsi walivyopambana.
“Lakini sasa tuko timamu na mawazo yetu yote yapo kwa wapinzani wetu. Ni timu nzuri, lakini na sisi si wabovu, kwa hiyo itakuwa mechi ya kujipanga sana,” alisema.
Pamba Jiji imetoka kupoteza dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-0, mechi iliyochezwa Aprili 11 katika michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora, hivyo inakwenda ugenini kwa TRA United kusaka matokeo mazuri.
Mechi hiyo itakayochezwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, inazikutanisha timu hizo zilizopishana pointi mbili, TRA ikiwa na 24, huku Pamba Jiji ikikusanya 26, zote zikicheza mechi 18.