KOCHA Msaidizi wa TMA FC ya jijini, Arusha, Omary Matwiko ‘Tico Tico’ amesema mazungumzo aliyofanya na Kocha Mkuu wa Yanga, Mreno Pedro Goncalves, yamemwongezea morali ya kupambana katika majukumu yake ili afikie malengo aliyojiwekea.
Matwiko anayefananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Msumbiji, Manuel Jose Luis Bucuane ‘Tico Tico’, amesema baada ya mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Yanga dhidi ya TMA, ndipo urafiki na Pedro ulipoanza.
“Baada ya mechi yetu na Yanga, Pedro alinifuata na kunipongeza kwa kazi kubwa niliyofanya, aliniuliza kuhusu elimu yangu na kushangazwa pia kuona timu ya Championship inacheza mpira mzuri kiasi kile, kiukweli ilinifariji,” amesema Tico Tico.
Aidha, Tico Tico amesema mbali na hilo, Pedro pia alimtaka kufundisha timu za vijana kwa sababu ni kocha mwenye uwezo mkubwa na bado ni mdogo, ingawa kwa anachokionyesha kitaleta manufaa makubwa katika karia yake ya ukocha baadaye.
Makocha hao walikutana katika mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora, iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Aprili 11, 2026 na TMA FC ilichapwa na Yanga bao 1-0.