Chama la Allarakhia lasaka ubingwa England

CHAMA la Mtanzania Tarryn Allarakhia, Rochdale AFC inayoshiriki Ligi Daraja la tano England (National League) ina kibarua kigumu cha kusaka ubingwa dhidi ya York City, itakayopigwa Jumanne, Aprili 21.

Timu hizo zimetofautiana pointi mbili, York City ikiwa kileleni na pointi 104 baada ya mechi 44, ikishinda 32 sare nane na kupoteza nne na imefunga mabao 110 hadi sasa.

Kwa upande wa Rochdale katika mechi 44 imeshinda 32, sare sita na kupoteza sita, huku ikifunga mabao 85 na ina pointi 102. Nafasi ya tatu ni Carlisle ikiwa na pointi 89.

Ligi hiyo yenye timu 24 kila chama linacheza mechi 48 na zimesalia nne kujua nani bingwa , huku ya Rochdale dhidi ya York City ndiyo itakayoamua.

Endapo Rochdale itashinda mechi hiyo, itafikisha pointi 106 na kuishusha York City kileleni Chama la Mtanzania huyo likishinda linafikisha pointi 106 na itaishusha York City iliyopo kileleni, huku ikijihakikishia kupanda Ligi Daraja la nne ‘EFL League Two’.

Hata hivyo, endapo itapoteza, italazimika kusubiri kucheza mtoano ‘play off’ kwani itakuwa na tofauti ya pointi 10 dhidi ya timu ya tatu.

Rekodi ya mechi 10 za mwisho zilipokutana timu hizo York City imeshinda mara sita, Rochdale mara moja na suluhu tatu.

Akizungumzia nafasi ya kupanda daraja Allarakhia amesema “Tunayo nafasi ya kupanda na kufanya vizuri kikubwa kuendelea kupambana kwa sababu siyo rahisi.”

Kiungo huyo mshambuliaji amecheza mechi 30 msimu huu akifunga mabao mawili na asisti mbili, huku msimu uliopita uliokuwa wa kwanza kwake alicheza mechi 43 na kufunga mabao manne.