BEKI wa kati wa Fountain Gate, Mrundi Derrick Mukombozi amesema licha ya kikosi hicho kutokuwa na mwenendo mzuri katika mechi za Ligi Kuu Bara, lakini malengo yao ni kuhakikisha timu hiyo inakwepa mtego wa kucheza mechi za ‘Play-Off’ msimu huu.
Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya juzi timu hiyo kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na kuhitimisha safari ya kucheza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi, tangu ilipoifunga Mbeya City bao 1-0, Machi 3, 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mukombozi amesema ushindi ilioupata timu hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar, umeongeza motisha zaidi ya kikosi hicho kufanya vizuri kwa mechi zijazo, ingawa jitihada zinahitajika kutokana na ushindani mkubwa uliopo sasa.
“Msimu uliopita tulikuwa katika presha kubwa sana ya kuibakisha timu Ligi Kuu, safari hii pia tupo nafasi za kucheza ‘Play-Off’, ingawa tunachopambana ni kuhakikisha tunaondoka chini tulipo na kukaa sehemu nzuri,” amesema Mukombozi.
Aidha, amesema mabadiliko ya mara kwa mara katika kikosi hicho hayawezi kuwaathiri kwenye utendaji wao kwa sasa, isipokuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaendelea kutoa ushirikiano kwa kila kocha atakayekuwa anawafundisha.
Ushindi huo wa Fountain Gate ni wa kwanza kwa Kocha, Fredy Felix ‘Minziro’, tangu ateuliwe Aprili 10, 2026, kuchukua nafasi ya Mohamed Ismail ‘Laizer’, aliyeondoka baada ya kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande zote hizo mbili.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Fountain Gate ilimaliza nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 29 na kucheza ‘Play-Off’ ya kubakia, ikianza kwa kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Tanzania Prisons, iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 31.
Baada ya hapo, Fountain Gate ikacheza tena ‘Play-Off’ ya mwisho ya kujinasua kushuka daraja na ilikabiliana na Stand United ya Championship, ikashinda jumla ya mabao 5-1 na kikosi hicho kubakia.
Timu hiyo iliyoanza msimu wa 2025-2026 kwa kufundishwa na makocha, Denis Kitambi, Mohamed Ismail ‘Laizer’ na sasa Fredy Felix ‘Minziro’, imecheza mechi 19 za ligi, ikishinda tano, sare nne na kupoteza 10, ikishika nafasi ya 13 na pointi 19.
