Marekani Yaitishia Iran: Hatutasita Kutumia Nguvu Endapo Haitatii Zuio la Baharini

Mkuu wa Majeshi wa Marekani Dan Caine (kulia) akiongea jambo akiwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth (kushoto).

Marekani imeongeza presha kwa Iran baada ya kutoa onyo kali kuwa iko tayari kutumia nguvu endapo haitatii zuio la baharini (blockade) lililowekwa katika eneo muhimu la Strait of Hormuz.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Majeshi wa Marekani Dan Caine alisema wazi kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa meli yoyote itakayokaidi amri hiyo. “Kama hutatii zuio hili, tutatumia nguvu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema jeshi la nchi hiyo lina uwezo wa kubadilika haraka kutoka operesheni ya kudhibiti bahari kwenda kwenye vita kamili muda wowote. Aliongeza kuwa lengo kuu la Marekani ni kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia, iwe kwa njia ya makubaliano au nguvu.

Zuio hilo linaathiri meli zote zinazoelekea au kutoka Iran, bila kujali taifa zinakotoka. Tayari baadhi ya meli zimeanza kubadilisha njia kwa hofu ya hatua za kijeshi, huku Jeshi la Marekani likisema halijalazimika bado kukamata meli yoyote.

Mvutano huu unakuja licha ya kuwepo kwa usitishaji wa mapigano wa muda kati ya Iran na Marekani, huku mazungumzo ya amani yakiendelea kusuasua kutokana na tofauti kubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Eneo la Strait of Hormuz ni muhimu sana duniani kwani hupitisha karibu sehemu kubwa ya mafuta ya dunia, jambo linalofanya mgogoro huu kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa kimataifa.

Wakati huo huo, Iran imejibu kwa vitisho, ikionya kuwa inaweza kushambulia meli za Marekani na hata kufunga njia nyingine muhimu ya bahari. Hali hii inaongeza hofu ya kurejea kwa vita kamili ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindwa.

Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kusisitiza kuwa anapendelea suluhisho la amani kupitia mazungumzo, lakini akaweka wazi kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua kali endapo makubaliano hayatapatikana.

Kwa sasa, macho ya dunia yameelekezwa katika maendeleo ya mazungumzo hayo, huku wengi wakihofia kuwa hali inaweza kubadilika ghafla na kuingia kwenye mgogoro mkubwa zaidi wa kijeshi.