Mgomo wa daladala Tanga waingia siku ya pili, usafiri bado wateteraka

Tanga. Hali ya usafiri wa daladala katika Jiji la Tanga bado haijaimarika kutokana na mgomo unaoendelea.

Mgomo huo umeendelea kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa jiji hilo, huku wananchi wengi wakijikuta wakikosa huduma muhimu ya usafiri wa kila siku.

Zaidi ya daladala 400 zimesimama kutoa huduma katika jiji hilo, hali hiyo imewaacha abiria wengi wakihangaika kufika katika maeneo yao ya kazi.

Mwananchi ilifika alfajiri katika kituo cha mabasi ya ndani ya jiji hilo na kushuhudia daladala chache zikiendelea kutoa huduma, huku abiria wakionekana kusubiri kwa muda mrefu bila mafanikio.

Mgomo huo ulianza Aprili 15, 2026, ukichochewa na kupanda kwa bei ya mafuta. Madereva wanalalamikia kushuka kwa kipato chao kutokana na gharama kubwa za uendeshaji, hali inayowafanya washindwe kuendelea na kazi zao za kila siku.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Tanga, Shedrack Malale, amesema juhudi zinaendelea kutafuta suluhu.

Amesema wamefanya vikao na wadau mbalimbali, wakiwemo madereva na wamiliki, kwa lengo la kuhakikisha huduma ya usafiri inarejea haraka.

“Tumekutana na wadau na kujadili changamoto zilizopo kati ya madereva na wamiliki,” amesema Malale.

Wakazi wa jijini Arusha wakipanda daladala eneo la Soko la Kilombero linalofanya safari zake kati ya Nelson Mandela na Mapambazuko jana. Picha na Filbert Rweyemamu

Ameeleza kuwa changamoto kubwa ni kiwango cha fedha kinachotakiwa kurejeshwa kwa wamiliki, akibainisha kuwa hali hiyo imechangiwa na kupanda kwa gharama za mafuta.

Malale amesema wameitisha kikao cha wamiliki wa daladala kujadili hali hiyo, na kwamba walikutana na viongozi wa madereva siku ya awali kwa majadiliano ya kina yaliyolenga kupata muafaka wa haraka.

“Tumekubaliana wamiliki wawavumilie madereva katika kipindi hiki cha mpito,” amesema Malale.

Ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza mvutano uliopo baina ya pande hizo, huku akisisitiza kuwa suluhisho la kudumu linaendelea kutafutwa.

“Huduma zinatarajiwa kuanza kurejea kuanzia mchana, huku tukisubiri maelekezo ya Serikali kuhusu nauli,” amesema, akiongeza kuwa mazungumzo yanaendelea ili kuhakikisha hali inatengemaa, huku akitoa wito kwa wadau wote kuwa na subira.

Katibu wa Umoja wa Daladala wilaya ya Tanga (Muwata) Mwang’ombe Hassan, ametoa rai kwa madereva kurejea kazini, akisema changamoto zilizopo zinafanyiwa kazi na zinahitaji utulivu wa wadau. Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

“Kipato cha madereva kimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kupanda kwa gharama,” amesema, akieleza kuwa wamiliki wanapaswa kuelewa hali halisi ya sasa ya uchumi, hali iliyochochea mgomo huo.

Dereva wa daladala, Salekhe Rajabu, amesema hali ya sasa ni ngumu kwao. Amesema mapato wanayopata hayaendani na gharama za mafuta na uendeshaji, hali inayowafanya washindwe kuendesha familia zao.

“Sasa hivi tunafanya kazi kama tunamtafutia mmiliki fedha, sisi hatupati chochote. Baada ya kuweka mafuta, hakuna kinachobaki. Hali hiyo haiwezi kuendelea kuvumilika,” amesema Salekhe.

Mwenyekiti wa Muwata Jijini Tanga, Salimu Jumbe, amesema wamiliki hawajagoma kutoa huduma, bali madereva ndio wamechukua hatua hiyo kutokana na hali ya kipato. Amesema mfumo wa mapato umekuwa changamoto kubwa.

Jumbe amesema dereva hulazimika kutoa Sh30,000 hadi Sh40,000 kwa mmiliki, baada ya hapo anaweka mafuta na kubaki bila faida yoyote, hali inayowakatisha tamaa madereva wengi.

Wananchi wa Jiji la Tanga wameiomba Serikali kutokubali kupandisha nauli. Wamesema hatua hiyo itaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kipato cha chini, wakieleza kuwa tayari wanakabiliwa na gharama kubwa za maisha.

“Tupo tayari kutembea kwa miguu, lakini Serikali isipandishe nauli,” amesema Bakari Mbwana.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, hakuzungumza kuhusu suala hilo, kupitia ofisi yake, alieleza kuwa yupo kwenye kikao kinachohusu mgogoro huo na ameahidi kutoa taarifa zaidi kesho, Aprili 17.