Mradi wa DREAMS Wawanufaisha Wananchi Tabora

Na Mwandishi Wetu, Tabora

Zaidi ya kaya 4,500 katika Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora, zimenufaika na mradi wa DREAMS Tanzania unaolenga kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, matumizi ya fursa zilizopo na utunzaji wa akiba kwa malengo ya muda mfupi, mrefu pamoja na kukabiliana na dharura.

Mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali vikiwemo Ulyankulu, Mishamo, Makingi na Katumba, ukiwa na lengo la kuimarisha uchumi wa kaya na mtu mmoja mmoja.

Akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Makazi ya Ulyankulu, Bw. Samwel Makungu, aliwahimiza washiriki kutumia kwa vitendo elimu waliyoipata ili iweze kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.

“Elimu hii iwasaidie kwa vitendo. Msiiache, endeleeni kuifanyia kazi kama mnavyofanya sasa. Tunataka kuona matajiri wakitokea katika maeneo haya, na hilo linawezekana kabisa,” alisema Bw. Makungu.

Aliongeza kuwa maeneo ya vijijini yana fursa nyingi za kiuchumi zikiwemo ufugaji, kilimo na biashara za mazao pamoja na bidhaa muhimu, ambazo zinaweza kuwapatia wananchi kipato cha kudumu.

“Mmefundishwa namna ya kutumia fursa zilizopo katika mazingira yenu ili kuongeza kipato cha familia zenu. Tayari mnaonekana kubadilika—watoto wanakwenda shule na maisha yenu yanaimarika,” aliongeza.

Kwa
upande wake, Meneja Msaidizi wa Mradi wa DREAMS Tanzania, Bw. Martine
Mgala, alisema mradi huo ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kutekelezwa
kwa kipindi cha miaka minne, huku hadi sasa ukifikia zaidi ya kaya
5,000.

“Kadiri mradi
unavyoendelea, tunatarajia kufikia kaya nyingi zaidi. Wananchi
wameupokea vizuri na tayari baadhi yao wanaanza kuona mabadiliko katika
maisha yao,” alisema.

Alieleza
kuwa changamoto kubwa iliyokuwepo awali ilikuwa ni ukosefu wa uelewa wa
namna ya kutambua na kutumia fursa zilizopo katika jamii, lakini kwa
sasa hali imeanza kubadilika.

“Wananchi
sasa wameamka, wanazitumia fursa zilizopo na wanaanza kukidhi mahitaji
yao ya msingi. Pia ushirikiano kati ya wazazi umeongezeka katika kuinua
uchumi wa familia,” aliongeza.

Baadhi
ya wanufaika wa mradi huo walieleza namna mafunzo hayo yalivyobadilisha
maisha yao. Bw. Shukuru Kabugire alisema wamepata mwamko mpya wa
kiuchumi na sasa wana uwezo wa kujikimu.

“Awali
maisha yalikuwa magumu sana, lakini sasa tumegundua kuwa fursa
zilikuwepo karibu nasi. Tunalima bustani na kila siku tunaingiza kipato.
Sina mawazo kama zamani,” alisema.

Naye
Bi. Ana Gervas, mkazi wa Kanindo Ulyankulu, alisema mradi wa DREAMS
umewasaidia kubadili mtazamo wao kuhusu maisha na kuwatoa katika hali ya
umaskini waliyoizoea.