Lindi. Wananchi wa Mkoa wa Lindi wanatarajiwa kunufaika na huduma bora na ya haraka ya umeme kufuatia Serikali kukabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Vifaa hivyo vimetolewa kupitia Wizara ya Nishati na kukabidhiwa kwa Tanesco Mkoa wa Lindi na Mkuu wa Mkoa huo, Zainab Telack, kwa niaba ya Serikali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutatua changamoto za upatikanaji wa umeme na kuendana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 16, 2026 baada ya makabidhiano hayo, Telack amesema ongezeko la vitendea kazi litaliwezesha shirika hilo kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi na kwa wakati.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme, ikiwemo kuunganisha vitongoji 526, ili kupanua upatikanaji wa nishati safi na kuchochea maendeleo huku ikilinda mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack (kushoto) akimkabidhi funguo za gari Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Theodory Hall (watatu kutoka kulia ), ishara ya kupokea vitendea kazi hivyo.Picha na Bahati Mwatesa.
“Mahitaji ya umeme mkoani Lindi yanaongezeka kwa kasi kutokana na uwepo wa miradi mikubwa ya maendeleo kama bandari ya uvuvi Kilwa, mradi wa gesi asilia (LNG) na shughuli za uchimbaji madini. Hivyo, ni muhimu huduma za umeme ziendane na kasi hiyo,” amesema Telack.
Amewataka Tanesco kuongeza juhudi katika utekelezaji wa miradi inayoendelea, kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa wa umeme na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary, amesema vitendea kazi hivyo vitaimarisha utendaji wa shirika hilo na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kushughulikia changamoto za wananchi.
Baadhi ya wananchi wa mjini Maswa ambao walipata majiko banifu ya kutumia mkaa kidogo kwa gharama nafuu.Picha na Samwel Mwanga
“Ni muhimu kuendeleza ushirikiano. Changamoto zikijitokeza, tushirikiane ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme,” amesema.
Naye Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi, Theodory Hall, amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni magari manne, bajaji saba, pikipiki 10 na kompyuta nane, ambavyo kwa pamoja vitasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa shirika hilo.
Ameahidi kuyatekeleza maelekezo yaliyotolewa na viongozi na kuhakikisha huduma ya umeme inaboreshwa ili kuwafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa.
