Samia atwaa tuzo, aeleza mapinduzi ya upasuaji ubongo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za kibingwa na kuongeza upatikanaji wa matibabu.

Akifungua mkutano wa pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya za Upasuaji wa Ubongo Duniani (WFNS), leo Aprili 16, 2026, Rais Samia amesema Tanzania imeongeza idadi ya hospitali zinazotoa huduma za upasuaji wa ubongo kutoka mbili zilizokuwepo miaka mitano iliyopita hadi saba kwa sasa.

Amesema hatua hiyo ni matokeo ya uwekezaji endelevu katika miundombinu ya afya na huduma za kibingwa, ukilenga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizo ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia amebainisha ongezeko kubwa la wataalamu wa afya nchini, akisema wataalamu wa tiba katika nyanja mbalimbali imepanda kutoka 138 mwaka 2020 hadi 1,518 mwaka 2026.

Kwa upande wa wataalamu wa upasuaji wa ubongo, amesema wameongezeka kutoka 12 hadi 37, ambapo saba kati yao ni wanawake ishara ya ongezeko la ushiriki wa wanawake katika fani za kitabibu zilizokuwa zikichukuliwa kuwa ngumu na za kiufundi zaidi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe Aprili 16, 2026.

“Mafanikio haya yanaonesha dhamira yetu ya kuimarisha uwezo wa kitaifa na kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wote,” amesema Rais Samia.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya afya kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na matumizi ya mifumo ya afya ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na uendelevu wa huduma.

Rais Samia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya tiba ya ubongo, akitoa wito kwa wataalamu na taasisi mbalimbali kuendelea kubadilishana ujuzi na teknolojia ili kuimarisha matokeo ya matibabu, hususan kwa magonjwa ya mfumo wa fahamu ambayo yanahitaji utaalamu wa hali ya juu.

Katika hatua nyingine, Rais ametunukiwa tuzo maalumu ya ubinadamu ya upasuaji wa ubongo kutokana na mchango wake katika kuimarisha huduma za afya na hususan upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea tuzo maalum ya ubinadamu ya upasuaji wa ubongo (humanitarian award) aliyokabidhiwa na Shirikisho la Jumuiya za Upasuaji wa Ubongo Duniani (WFNS) kutokana na mchango wake katika kuimarisha huduma za afya hususan upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu nchini.  

Akikabidhi tuzo hiyo, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania, Dk Othman Kiloloma, amesema uongozi wa Rais Samia umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, hasa katika kuokoa maisha ya wagonjwa wa magonjwa ya ubongo na uti wa mgongo.

“Kwa niaba ya wataalamu wa upasuaji wa ubongo na mgongo, tunatambua na kushukuru mchango wako mkubwa wa kibinadamu. Tuzo hii ya ubinadamu ya upasuaji wa ubongo ni ishara ya heshima kwa uongozi unaoweka utu wa binadamu mbele,” amesema Dk Kiloloma.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema idadi ya hospitali zinazotoa huduma za ubongo na mishipa ya fahamu imeongezeka kutoka mbili miaka mitano iliyopita hadi saba kufikia Aprili 2026, hatua inayoonyesha uwekezaji endelevu katika miundombinu ya afya.

“Ongezeko hili linaonesha dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, unaotarajiwa kuibua mapendekezo ya kuboresha huduma za dharura, kinga na matibabu ya haraka, sambamba na kuimarisha mtandao wa wataalamu barani Afrika.

Mchengerwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika vituo vya kisasa vya tiba kama Kituo cha Sayansi ya Mishipa ya Fahamu cha Mloganzila, upanuzi wa huduma katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), pamoja na kuanzishwa kwa teknolojia za kisasa za uchunguzi na vituo vya urekebishaji.

Akizungumzia changamoto za afya nchini, Mchengerwa amesema ajali za barabarani na magonjwa yasiyoambukiza kama kiharusi bado ni tatizo kubwa linalochangia idadi kubwa ya wagonjwa.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya majeraha ya ubongo husababishwa na ajali, hususan za bodaboda, ambapo kati ya watu 10 wanaopata ajali, takriban watatu hupata ulemavu wa kudumu.

“Changamoto hizi zinahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu na usafirishaji ili kuimarisha usalama barabarani na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika,” amesisitiza.