Mbeya. Wajasiriamali wa Soko la Rujewa wilayani Mbarali wameiomba Serikali kuharakisha maboresho ya miundombinu ya Barabara ya Igawa–Rujewa wakieleza kuwa hali yake imekuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa biashara na uchumi wa eneo hilo.
Ombi hilo limewasilishwa katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika Aprili 16, 2026 katika kituo cha mabasi Rujewa, ulioratibiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya watendaji kuwafikia wananchi.
Mbali na barabara, wafanyabiashara hao pia wameomba kuchimbwa kwa mifereji ya maji ya mvua ndani ya kituo cha mabasi, wakisema changamoto hiyo imekuwepo kwa muda mrefu na kuathiri shughuli za biashara hasa nyakati za mvua.
Wakizungumza katika mkutano huo, wajasiriamali wamesema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutasaidia kuvutia wafanyabiashara kutoka maeneo mengine, kuongeza mzunguko wa biashara na kukuza mapato ya Serikali.
Mjasiriamali Maclina Mbilinyi amempongeza mkurugenzi huyo kwa kuanzisha utaratibu wa kusikiliza wananchi, akisema umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Mbarali.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, Raymond Mweli akijibu kero za wananchi wakiwepo wafanya biashara katika kituo cha mabasi Rujewa wilayani humo. Picha na Hawa Mathias.
“Kwa miaka mingi tulikuwa na changamoto nyingi, lakini kwa muda mfupi mambo yameanza kubadilika ikiwemo kuboreshwa kwa kituo cha mabasi na ujenzi wa miundombinu ya vyoo vya kisasa,” amesema Mbilinyi.
Aidha, ameiomba kuruhusiwa kwa usafiri wa bajaji kuingia ndani ya kituo cha mabasi ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na bidhaa pamoja na kuondoa biashara zisizo rasmi zinazofanyika nje ya eneo hilo.
Mfanyabiashara mwingine, Nuhu Juma amesema mikutano ya kusikiliza kero imefungua ukurasa mpya wa mawasiliano kati ya wananchi na viongozi, hatua iliyorejesha imani kwa Serikali.
“Hatukuwa na utaratibu kama huu kwa muda mrefu. Sasa tunaona matumaini ya Mbarali mpya,” amesema Juma.
Kwa upande wake, Sakina Joel ameomba kuboreshwa kwa huduma ya maji safi, akisisitiza umuhimu wake katika kulinda mazingira na kuhakikisha miradi ya vyoo inafanya kazi kwa ufanisi.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Raymond Mweli, amesema suala la ubovu wa barabara ya Igawa–Rujewa tayari limewasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.
Amesema halmashauri imetenga zaidi ya Sh900 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kisasa wa matengenezo ya barabara ili kukabiliana na changamoto za miundombinu kwa haraka.
“Sasa hatutasubiri tena mamlaka nyingine pekee, tutakuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto za barabara ndani ya wilaya yetu,” amesema Mweli.
Mweli ameongeza kuwa ameanzisha ratiba ya ziara za kila wiki katika kata zote ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi moja kwa moja, akieleza kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kutoweka utendaji ofisini pekee.
Kuhusu ombi la bajaji kuingia ndani ya kituo cha mabasi, amesema atalifanyia kazi kwa kushirikiana na uongozi wa kata ili kupata suluhisho litakalowanufaisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa halmashauri itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kukuza uchumi wa wananchi wa Mbarali.
Mweli ametumia nafasi hiyo kutoa fursa kwa wananchi kuchamkia mikopo asilimia 10 ya wanawake, vijana na walemavu na kubainisha zaidi ya Sh2.2 bilioni zimetolewa.
“Maofisa maendeleo watapita huko, mpaka sasa tuna kiasi cha zaidi ya Sh600 milioni zipo kwenye halmashauri zinasubiri wakopaji,”amesema.
