Wahimizwa kuwekeza nguvu uwekezaji huduma za maji vituo vya afya

Dar es Salaam. Wabunge wamehimizwa kuharakisha uwekezaji katika huduma za maji, usafi na usafi wa mazingira (WASH) katika vituo vya afya, kufuatia ushahidi mpya unaoonesha kuwa mazingira duni ya kujifungulia yanaweka maisha ya maelfu ya akina mama na watoto wachanga hatarini.

Wito huo umeibua dhamira ya wabunge kusimamia mageuzi yatakayopunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika.

Katika kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika Dodoma jana, WaterAid Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo TAWASANET, Water For People na Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), walikutana na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi, wakisisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele huduma za WASH katika vituo vya afya.

Kikao hicho kilichowakutanisha wabunge 12 kililenga kuongeza uelewa kuhusu mchango wa huduma za WASH katika kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga, mtoto na balehe (RMNCAH), hususan wakati wa kujifungua.

Katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, takribani wanawake 36 hufariki kila siku kutokana na sepsisi ya uzazi maambukizi yanayohusishwa kwa kiwango kikubwa na mazingira yasiyo safi wakati wa kujifungua.

Wanawake katika ukanda huo wako katika hatari ya kufariki kwa sepsisi kwa kiwango cha juu zaidi mara 150 ikilinganishwa na wale wa nchi zenye kipato cha juu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Born Without Water, takribani asilimia 94.4 ya wodi za wazazi hazina huduma za msingi za usafi wa mazingira.

Aidha, mapungufu yanaonekana katika usimamizi wa taka (asilimia 68), uwepo wa vituo vya kunawa mikono (asilimia 58), usafi wa mazingira (asilimia 55) na upatikanaji wa maji safi (asilimia 45).

Upungufu huu hauathiri tu maisha ya akina mama na watoto wachanga, bali pia unadhoofisha uwezo wa wahudumu wa afya kutoa huduma salama, zenye staha na ubora unaohitajika.

Mkurugenzi wa Nchi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema huduma bora za afya haziwezi kupatikana bila uhakika wa maji safi na huduma za usafi.

“Huwezi kujenga mfumo imara wa afya juu ya msingi dhaifu. Mama anayejifungua bila maji safi au huduma za msingi za usafi ni mfumo unaomwangusha,” amesema Anna.

Ameongeza kuwa uwepo wa wataalamu, dawa na vifaa tiba vya kisasa hauwezi kutoa matokeo yanayotarajiwa iwapo huduma za WASH hazitapewa kipaumbele, kwani huathiri usalama, staha na ubora wa huduma.

Ameongeza kuwa WaterAid Tanzania ilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Bunge pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha huduma za WASH zinaunganishwa kikamilifu katika mipango ya afya ya mama na mtoto.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi, Dk Johannes Lukumay amekiri kuwa wanawake na wasichana hubeba mzigo mkubwa zaidi pale upatikanaji wa maji unapokuwa mdogo.

Amesema Tanzania inalenga kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji safi ifikapo mwaka 2030, lakini akaonya kuwa huduma duni bado zinachochea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara.

“Nimeshuhudia utekelezaji wa miradi ya WaterAid, ikiwemo Geita, ambapo muuguzi alilazimika kwenda kuchota maji wakati akihudumia wagonjwa. Leo, kutokana na uwekezaji katika WASH, maji safi yanapatikana kwa urahisi,” amesema.

Naye Meneja wa Athari na Ushawishi wa Kitaifa wa Water For People, Rose Riwa, amesisitiza kuwa huduma za WASH zina uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa.

“Hatuwezi kufikia Dira ya Taifa ya 2050 ikiwa watoto wataendelea kuugua mara kwa mara na kukulia katika mazingira yasiyo salama kiafya,” amesema.